Habari za Kitaifa

Kamati ya Bunge yaidhinisha Mswada kulazimisha huduma za serikali kukubali pesa taslimu

Na SAMWEL OWINO July 31st, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KAMATI moja ya Bunge imeidhinisha mswada kielelezo unaolenga kulazimisha biashara zote kukubali pesa tasilimu kama njia ya kulipia bidhaa na huduma.

Kamati ya Bunge kuhusu Fedha imependeza uchapishaji ya Mswada wa Marekebisho ya Sheria ya Benki Kuu ya Kenya, 2025.

Mswada huo unalenga kuifanyia Marekebisho Sheria ya Benki ya Kenya, Sura ya 291 kuhakikisha kuwa malipo kupitia pesa taslimu yakubalika hata wakati wa kulipia huduma za serikali.

“Mswada huo unazitaka biashara zinazouza bidhaa na huduma zikubali malipo ya pesa taslim ya hadi Sh100,000. Vile vile, unazuia biashara mbalimbali kutoza bei ya juu kwa wanunuzi wanaolipa kwa pesa taslimu na hivyo kuendeleza haki katika malipo,” inasema pendekezo hilo.

Kamati hiyo ya Fedha ilipokutana na mdhamini wa Mswada huo, Caroli Omondi, ilitaja pendekezo hilo kama nzuri na ikasema itapendekeza kuchapishwa rasmi kwa mswada huo ili ujadiliwe rasmi bungeni.

Naibu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Benjamin Langat aliyeongoza kikao kilichoidhinizwa mswada huo, alisema ni kinyume cha sheria kukataa pesa taslimu kama njia ya malipo.

“Tutawasilisha pendekezo kwa Spika kwamba Mswada huo uchapishwe baada ya kufanyiwa marekebisho kadhaa,” Bw Langat akasema.

Bw Langat alisema kuwa biashara zote sharti zihakikisha kuwa njia zote za malipo zinatumika na hakuna mwanamume anayenyimwa haki.

“Njia zote za malipo ziruhusiwe ili nikitaka kulipa kwa kutumia kadi ya malipo, pesa taslim, au Mpesa, nitaweza kusaidiwa,” Bw Langat akasema.

“Wale wafanyabiashara wanaokataa malipo ya pesa taslimu wanawakosea hawa watu wanaoishi na ulemavu,” akasema Mbunge wa Homa Bay Mjini Peter Kaluma.

Kamati hiyo pia iliidhinishwa faini ya Sh100,000 kwa wafanyabiashara ambao watakataa kukubali malipo kwa njia ya pesa taslim.

Hata hivyo, Kamati hiyo imependekeza mabadiliko kadhaa kwa mapendekezo kwenye mswada huo ambayo wanataka yashirikishwe katika ripoti yao kabla ya mswada huo kuchapishwa.

Kwa mfano, wanachama wa Kamati hiyo wanataka biashara zinazohudumu katika maeneo yanayozongwa na utovu wa usalama kuruhusiwa kutokubali malipo ya pesa taslim.

Ili kupunguza visa vya ufisadi na kuimarishwa kwa shughuli ya utoaji huduma za serikali, Kamati hiyo ilipendekeza kuwa vituo vya Huduma Centres viendelee kuruhusu malipo kwa njia ya simu pekee wala sio pesa taslim.

Isitoshe, Kamati hiyo ya Fedha pia inataka malipo ya pesa nyingi kuanzia Sh500,000 kwenda juu ziruhusiwe kufanywa kwa njia isiyo ya pesa taslim.

Mbunge wa Turkana Kusini John Ariko alisema ili kuimarisha uwazi haswa katika serikali na biashara mbalimbali, malipo yasiyo ya pesa taslim yaendelee kuruhusiwa.

TAFSIRI: CHARLES WASONGA