Habari za Kitaifa

Kamati ya sheria ya seneti yapinga muhula wa rais kuongezwa

Na MARY WANGARI November 2nd, 2024 Kusoma ni dakika: 2

KAMATI ya Seneti kuhusu Haki na Masuala ya Sheria inayoongozwa na Seneta wa Bomet, Hillary Sigei, sasa inaitaka Seneti isipitishe Mswada unaopendekeza kuongezwa kwa muhula wa Rais na viongozi waliochaguliwa.

Mswada wa Marekebisho ya Katiba uliowasilishwa na Seneta wa Nandi Samson Cherargei unapendekeza muhula wa kuhudumu wa rais, maseneta, magavana na wabunge kuongezwa kutoka miaka mitano hadi saba.

Kamati hiyo ilisema kwamba Wakenya wengi wamepinga pendekezo hilo.

“Kamati ya Seneti kuhusu Haki, Masuala ya Sheria na Haki za Kibinadamu inapendekeza kuwa Seneti isipitishe Mswada wa Marekebisho kuhusu Katiba ya Kenya nambari 2, 2024, Miswada ya Seneti, Nambari 46 ya 2024,” ilisema katika ripoti.

Aidha, Kamati hiyo imeagiza Kamati ya Seneti kuhusu Taratibu na Sheria iangazie upya mchakato unaoruhusu kujadiliwa kwa pendekezo la kisheria kuhusu kufanyia Katiba marekebisho ikiwemo kuanzisha marekebisho kwa kanuni za seneti.

“Pendekezo kama hilo litahitajika kuwa na saini ya angalau maseneta 15 wanaoliunga mkono, isipokuwa tu linapowasilishwa na Walio Wengi au Walio Wachache.”

Katika ripoti yake, kamati ilisema ilipokea barua pepe kutoka kwa maelfu ya Wakenya wakipinga vikali pendekezo la kuongeza muda wa hatamu za urais na viongozi waliochaguliwa.

Kufikia mwisho wa mchakato wa kushirikisha umma wiki iliyopita, jumla ya maoni 168, 801 yalikuwa yamepokewa kupitia baruapepe huku idadi kubwa ya raia wakipinga vikali mswada huo.

“Asilimia 99.99 ya maoni yaliyopokewa yalipinga vikali mswada huo wote kwa jumla au vipengele vilivyohusu kuongezwa muda wa kuhudumu wa rais, wabunge, magavana, na madiwani kutoka miaka mitano hadi saba,” ilisema Kamati hiyo kupitia kwa ripoti.

“Kufikia mwisho wa kushirikisha umma Ijumaa, Oktoba 25, 2024, wote walipinga vikali na kuirai Kamati kukataa Mswada huo isipokuwa mdau mmoja aliyezungumza akiunga mkono mswada.”

Ripoti hiyo iliorodhesha zaidi ya wadau 100 waliotoa maoni yao kupinga Mswada huo waliojumuisha: watu binafsi, afisi huru na za kikatiba, wabunge, maseneta, mashirika ya mabunge ya kaunti, makundi ya kidini, makundi ya vijana, wanawake na wanaharakati.

“Japo hayakuwasilishwa rasmi kwa Kamati kupitia mkondo uliohitajika, Kamati vilevile ilizingatia, mijadala ya kina ya umma kuhusu mswada huo iliyofanyika kwenye vituo vikuu vya habari na mitandao ya kijamii,” yasema ripoti.