Kambi ya Sifuna yachemkia Gachagua kwa kuwaita ‘miradi’ na ‘fuko’ wa Ruto
MUUNGANO wa Kenya Moja ukiongozwa na Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna umemshutumu vikali aliyekuwa Naibu wa Rais Rigathi Gachagua kwa kuwarejelea viongozi wengine wa upinzani kama miradi ya serikali.
Bw Sifuna alisema kuwa upinzani uko kwenye hatari ya kuvunjika iwapo cheche kali zinazowakosea viongozi wengine heshima, zitaendelea kutolewa na viongozi kama Bw Gachagua.
Seneta huyo wa Nairobi alisema kuwa upinzani unastahili kudhamiria kumfurusha Rais William Ruto madarakani mnamo 2027 badala ya Bw Gachagua kukesha akiwakashifu viongozi wengine ili kutimiza maslahi yake ya kisiasa.
Akiongea na Taifa Leo, seneta huyo alipinga dhana kuwa kuna kundi la viongozi wa upinzani ambao wana uwezo wa kumng’atua Rais Ruto 2027 akisema wote wanastahili kushirikiana, na bila umoja, nia yao itakosa kufaulu.
“Kama viongozi chipukizi, tunasikitishwa na matamshi ya kugawanya yanayotolewa na baadhi ya viongozi wa upinzani. Wakenya wengi wanamtaka Rais Ruto ahudumu kwa muhula mmoja wala si baada ya 2027,” akasema Bw Sifuna.
Kwake, ni kinaya kwa baadhi ya viongozi kama Bw Gachagua kudai wanaitia mizani serikali huku wakiwarejelea wengine kama fuko na miradi ya uongozi wa sasa.
“Baadhi yetu tulikuwa tunashinikiza Ruto aende mnamo 2023 wakati Gachagua bado alikuwa naye serikalini. Ni lini sasa Gachagua mwenyewe ndiye amekuwa mdhamini wa pekee wa Ruto kutochaguliwa 2027?’’ akauliza Bw Sifuna.
“Kile tunahitaji ni umoja wala si kauli ya kuwarejelea viongozi wengine kama fuko,” akaongeza.
Kenya Moja inawajumuisha viongozi chipukizi kutoka mirengo yote ya kisiasa na imesisitiza kuwa haiegemei au kutegemea upinzani au Serikali Jumuishi katika siasa zake.
“Wakenya wasihadaike kuwa serikali ya sasa na upinzani, ndio pekee mirengo inayolenga kuupata uongozi wa nchi. Watu ambao ni bora kuliko William Ruto ni mamilioni nchini kwa hivyo, hatuwezi kuwekewa masharti ya kuwa na hiari ya kuwachagua kati ya viongozi watano pekee,” akasema.
Alikuwa akiwarejelea Rais Ruto, Bw Gachagua, Kalonzo Musyoka (Wiper), Eugene Wamalwa (DAP-K) na Kiongozi wa PLP Martha Karua.
Mnamo Jumapili, Bw Gachagua kwenye mahojiano na KTN alisema kuwa Rais Ruto alikuwa amewatuma fuko ndani ya upinzani ili kusambaratisha na kuwachanganya kuelekea kura ya 2027.
“Ameingilia upinzani na vyama vyetu na kuna wanasiasa anaowatumia kututatiza. Tumewaambia viongozi wawe makini,” akasema Bw Gachagua ambaye ni kiongozi wa DCP.
Naibu Kiongozi wa DCP Cleophas Malala juzi alikashifu Jubilee ya Rais Uhuru Kenyatta kama kati ya vyama vinavyotumiwa na serikali kutatiza uthabiti wa Bw Gachagua katika siasa za Mlima Kenya.
“Jubilee inastahili kuonywa isisababishe fujo iwapo kweli wao ni sehemu ya muungano wa upinzani,” akasema Bw Malala.
Alidai kuwa Jubilee ilikuwa inashirikiana na UDA kichinichini akisisitiza haimtakii mema Bw Gachagua kwenye siasa za nchi.
Hata hivyo, Katibu Mkuu wa Jubilee Jeremiah Kioni alimshutumu Bw Gachagua kwa kujaribu kumlazimisha aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiangí ahame Jubilee.
Kwa mujibu wa Bw Kioni, Bw Gachagua hata alimwaamrisha Dkt Matiangí aachane na Jubilee na badala yake abuni chama cha kisiasa chenye mizizi yake na uungwaji mkono kutoka eneo la Gusii.
“Yeye ndiye mradi wa Rais Ruto na anawahadaa Wakenya,” akasema Bw Kioni.
Kinachoendelea kwa sasa upinzani ni sawa na kile kilichofanyika kuelekea uchaguzi wa 1992, ambao ulikuwa wa kwanza baada ya mfumo wa vyama vingi kukumbatiwa.
Viongozi wa upinzani wakati huo Kenneth Matiba, Oginga Odinga, Masinde Muliro, Martin Shikuku, Charles Rubia miongoni mwa wengine walikuwa ndani ya FORD.
Hata hivyo, muungano huo ulipasuka Bw Oginga akiishia kuongoza Ford Kenya naye Bw Matiba akiwa nyapara wa Ford Asili.
Kwa upande mwingine Mwai Kibaki ambaye alikuwa amekosana na utawala wa KANU na kutimuliwa kama makamu wa rais, alibuni DP na kuenda nayo hadi debeni.
Mgawanyiko huo ulimwezesha Rais Daniel Moi kurejea madarakani.
Vivyo hivyo, katika kura ya 1997, upinzani ulishindwa kuungana na Mzee Moi akarejea tena madarakani.