Habari za Kitaifa

Kampuni ya kutafiti dhahabu ya Uingereza yakataliwa na wakazi

May 25th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA SHABAN MAKOKHA

KAMPUNI ya utafiti wa dhahabu ya Uingereza, Shanta Gold, inakabiliwa na upinzani kutoka kwa wenyeji kwenye Ukanda wa Lirhanda kwa tuhuma kuwa ina ajenda fiche hasa kutokana na jinsi inavyoendesha shughuli zake.

Wenyeji wanashutumu kampuni hiyo kwa kuchukua sampuli ya madini ya dhahabu katika eneo hilo bila kutoa matokeo yake.

Wanadai kuwa kampuni ya Shanta Gold inashindana na maelfu ya wenyeji ambao wanategemea uchimbaji wa madini kujikimu kimaisha.

“Wazazi wangu walikuwa wakitegemea shughuli hii. Leo hii nina familia yangu na sijawahi kufanya kazi nyingine yoyote ila hii ya uchimbaji madini. Hiki ndicho chanzo pekee cha mapato ambayo familia yetu inaitegemea. Iwapo Shanta Gold itashindana nasi, basi tutaendelea kuangamia,” akaeleza Bw John Aliero, mkazi wa eneo la Isulu huko Ikolomani.

Kampuni hiyo ya Shanta Gold inasema kuwa kuna dhahabu yenye thamani ya Sh171 bilioni kwenye ukanda wa Isulu-Bushiangala unaopakana na Ikolomani kupitia eneo bunge la Shinyalu.

Maeneo yenye madini mengi ya dhahabu kwenye ukanda wa Lirhanda ni pamoja na Malinya, Rosterman, Shirumba, Kilingili (kando ya Mto Iguhu), Shipeso, Isulu, Bushiangala na Sigalagala.

Ripoti ya Shanta Gold ilionyesha Kakamega pekee ina dhahabu yenye thamani ya Sh200 bilioni huku eneo la Ramula-Mwibona lililo kwenye mpaka wa maeneobunge ya Luanda na Gem katika Kaunti za Vihiga na Siaya ikiwa na dhahabu ambazo thamani yake inakadiriwa kuwa Sh61.81 bilioni.

Hata hivyo, wakazi wa maeneo hayo wanadai kuwa kampuni hiyo ina ajenda fiche.

Mapema mwaka 2024, Gavana wa Kakamega Fernandes Barasa aliitaka kampuni hiyo kusitisha shughuli zake hadi pale miongozo ifaayo inayobainisha masharti ya wazi ya ushirikiano kati ya kampuni hiyo na wenyeji itakapotungwa.

Gavana aliagiza kampuni hiyo kusitisha shughuli na kushirikisha utawala wake ili kukubaliana jinsi wakazi wangenufaika na biashara ya kusafisha dhahabu.

Kulingana na gavana Barasa, ishara hiyo ilikusudiwa kuoanisha masilahi ya mwekezaji na juhudi za kitengo kilichogatuliwa kuweka uwiano kati ya maendeleo ya kiuchumi na kulinda maslahi ya wenyeji.