Habari za Kitaifa

Kampuni za kibinafsi zapewa wiki moja kuongeza walinzi mishahara

January 29th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA MARY WAMBUI

KAMPUNI za kibinafsi zinazotoa huduma za ulinzi zimepewa siku saba kutii sheria ambayo imetoa mwongozo mpya wa mshahara wanaostahili kulipwa walinzi.

Kwa mujibu wa Mamlaka inayodhibiti Kampuni za Kibinafsi za Ulinzi (PSRA), walinzi ambao wanahudumu Nairobi wanastahili kulipwa mshahara usiopungua Sh30,000 huku wanaohudumu kaunti za nje wakipokea ujira usiopungua Sh27,183.

Isitoshe, wakurugenzi wa kampuni hizo za ulinzi watahitajika kutoa ushahidi na ithibati kuwa wamewalipa walinzi wao pesa hizo.

Ushahidi huo utakuwa kupitia kuwasilisha nakala ya stakabadhi ya malipo kila mwisho wa mwezi (payslip).

Kukosa kufuata mwongozo huo mpya wa mshahara utasababisha kampuni hizo kujipata motoni kisheria.

Kampuni zitakazokosa kutii sheria hiyo zitapigwa faini na pia leseni zao za kuhudumu zitafutiliwa mbali.
“Kampuni yoyote inayotoa huduma za ulinzi ambayo haitawasilisha stakabadhi za kisheria za kufuata mwongozo mpya wa mshahara, itapokonywa leseni,” ikasema PSRA.

Aidha, kampuni hizo hazitaficha idadi ya walinzi walioajiriwa kwa sabau PSRA inataka orodha ya walinzi hao ili wasajiliwe na kupokezwa nambari maalum.

Hatua hii mpya imechukuliwa na serikali ili kudhibiti sekta hiyo ambayo ni muhimu nchini.

Hata hivyo, kuna wasiwasi kuwa mwongozo huu mpya ukitekelezwa, kampuni nyingi zinazotoa huduma za ulinzi, zitasambaratika na kutoka kwenye biashara.

Miaka miwili iliyopita, Wizara ya Leba iliamrisha kuwa walinzi wanaofanya kazi katika miji mikuu Nairobi, Kisumu, Mombasa na Nakuru walipwe mshahara usiopungua Sh16,959.

Chini ya mwongozo wa wizara ya Leba, walinzi ambao watakuwa wakifanya kazi katika miji ambayo zamani ilikuwa manispaa, wanastahili kulipwa Sh15,722.

Wenzao katika miji mingine wanastahili kupokea Sh9,672 kila mwezi.

Mnamo Novemba 2023, usimamizi wa kampuni za usalama Kaskazini mwa Bonde la Ufa, ulielekea mahakamani kupinga mwongozo mpya wa mshahara.

Walifanikiwa kupata amri ya kuzuia PSRA kutekeleza mwongozi huo hadi kesi hiyo isikizwe na iamuliwe. Baadaye waliondoa kesi hiyo na faili ikafungwa.

Chini ya mwongozo mpya, walinzi wanastahili kulipwa Sh18,994, marupurupu ya nyumba ya Sh2,849.11 na pia marupurupu mengine ya Sh8,156.81

Pesa hizo kwa jumla ni mshahara wa Sh30,000 kila mwezi.