Habari za Kitaifa

Kampuni zashtaki JSC kwa ‘maamuzi ya kifisadi’ ya majaji yaliyozigharimu Sh8 trilioni

Na JOSEPH WANGUI September 25th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

KAMPUNI tatu za teknolojia zimeshtaki Tume ya Huduma ya Mahakama (JSC) kwa madai ya uzembe na udanganyifu wa majaji 10 katika utatuzi wa mzozo wa ajira uliochangia hasara.

Zinadai Sh8 trilioni kama fidia kwa kupoteza biashara na mali kupigwa mnada.

Kesi hii isiyo ya kawaida katika Mahakama Kuu ya Milimani, Nairobi, inaonyesha kwamba Skytop Technologies Limited, Skytop Mcarfix Limited na Demoscad Limited zinataka JSC kulipa fidia kwa hasara ya biashara na mali.

Sh8 trilioni ambazo ni mara mbili ya bajeti ya kitaifa ya Kenya ni dai ambalo halijawahi kushuhudiwa katika kesi mahakamani.

Watafiti wa sheria wanasema ingawa madai ya uzembe wa majaji ni mazito, kesi za fidia za matrilioni ya pesa ni nadra sana.

JSC, chini ya uenyekiti wa Jaji Mkuu Martha Koome, imepinga kesi hiyo, ikisema haiwezi kuadhibiwa kwa maamuzi ya majaji.

“Kuruhusu JSC kuwajibika kwa maamuzi ya mahakama au utendaji wa kawaida wa jopo la mahakama kunaweza kuhatarisha uhuru wa mahakama na kuathiri kazi ya kikatiba ya Mahakama na Tume,” JSC ilisema katika majibu yake.

JSC kupitia Msajili wa Usimamizi, Isaac Wamaasa, imeomba mahakama kuwa na tahadhari na kuepuka kubadilisha malalamishi ya utendaji kuwa michakato ya kiraia.

Walalamishi wamewasilisha malalamishi mbalimbali dhidi ya majaji wa tofauti ambao wameorodheshwa katika hati ya kesi.

Hata hivyo, majina yao hayawezi kutajwa hadharani kwa sababu hawajatajwa rasmi kama washtakiwa; kesi imefunguliwa dhidi ya JSC kama mwajiri wao.

Wadai kwamba Jaji Mkuu Koome hakuchukua hatua dhidi ya majaji au wafanyakazi wa mahakama waliodaiwa kufanya maamuzi ya kupendelea kitendo ambacho wanasema kinakiuka kiapo chake cha afisi.