Kanisa Eaglerise Christian laendelea kufungwa mzozo ukitokota
Mgogoro wa uongozi ulioshuhudiwa katika Kanisa la Eaglerise Christian, Athi River, siku ya Jumapili umechukua mkondo mpya huku pasta anayepigwa vita, Nahashon Wambua Mwangangi, akiahidi kutoliruhusu kanisa hilo liondoke mikononi mwake.
Akiwa na amri kutoka Mahakama Kuu ya Machakos inayowazuia wajumbe wa baraza la kanisa hilo kuingilia masuala yake, Pasta Mwangangi alisema hakuna mtu aliye na mamlaka ya kimaadili kumfurusha kutoka kanisa alilolianzisha peke yake mwaka wa 2009.
Alisema wale wanaomshinikiza aondoke hawajawahi hata kuchangia senti moja katika ununuzi wa ardhi au ujenzi wa kanisa hilo.
“Mimi ndiye mwanzilishi wa kanisa hili mwaka wa 2009. Nilianza katika nyumba ya rafiki, baadaye nikapangisha ardhi hii, nikainunua na kujenga kanisa. Tumekuwa hapa kwa miaka 16 sasa,” alisema.
Alikuwa akijibu kauli ya Askofu wa Eaglerise Christian Church, Leonard Wambua, aliyedai kuwa Mwangangi si mchungaji wa kanisa hilo tena na kwamba mtu mpya, Emmanuel Kioko, ndiye amechukua nafasi hiyo.
“Kama kanisa, hatuwezi kuachilia mahali ambapo tulinunua ardhi na kujenga kanisa. Eaglerise haikuwahi kutoa hata senti moja kwa ununuzi wa ardhi au ujenzi wa kanisa,” Mwangangi alisisitiza. “Hii ni njama ya kupora waumini mali yao.”
Mwangangi aliwataja Wambua na Kioko kama “wageni” si tu kwa kanisa hilo, bali pia kwa jamii ya Athi River ambapo kanisa hilo limehudumu kwa zaidi ya muongo mmoja.
Kanisa hilo lililoko katika kituo cha biashara cha Makadara, ndani ya mji wa Athi River, lilifungwa kwa muda usiojulikana baada ya vurugu kuzuka Jumapili kutokana na mzozo wa uongozi.
Tangu siku hiyo, kanisa limeendelea kufungwa. Hakuna ibada iliyofanyika siku hiyo huku waumini wakigawanyika katika pande hasimu.
Maafisa wa polisi kutoka kituo cha Athi River waliingilia kati na kurejesha utulivu kabla ya kanisa kufungwa hadi suluhu ipatikane.
Baadhi ya waumini walikuwa wakipiga kelele nje ya kanisa wakati mwandishi huyu alifika eneo hilo mwendo wa saa nane na nusu mchana Jumapili. Milango ya kanisa ilifungwa kwa amri ya polisi.
Ingawa Mwangangi alikuwa na agizo kutoka Mahakama Kuu ya Machakos linalowazuia viongozi wa kanisa kuingilia mambo ya kanisa hilo, mahakama ya Mavoko ilimzuia yeye mwenyewe kuingia katika majengo ya kanisa.
“Kuna amri ya mahakama inayomzuia mchungaji wa kanisa hili (Nahashon Wambua Mwangangi) kuingia kanisani. Leo tulikuja kumtambulisha mchungaji mpya, Emmanuel Kioko, lakini inaonekana kama Mwangangi aliyekuwa amezuiwa alikusanya kundi lake,” alisema Askofu Wambua.
Kwa mujibu wa Mwangangi, mzozo huo ulianza kushika kasi mwezi Juni mwaka huu, wakati Wambua alimleta Kioko kumrithi kama mchungaji. Hata hivyo, Kioko alikataliwa na waumini.
“Wambua anataka niondoke kwa sababu hatukubaliani jinsi anavyoendesha kanisa la Eaglerise. Tulishirikiana awali kama washirika wa huduma, lakini sasa anaonyesha kuwa ajenda tofauti,” alisema Mwangangi, akisisitiza kuwa hataachilia kanisa kwa urahisi.