Kanisa Katoliki lakataa mamilioni ya Ruto, lasema pesa zilizotolewa zitarudishwa
ASKOFU Mkuu wa Kanisa Katoliki Dayosisi wa Nairobi Philip Anyolo ameagiza Rais William Ruto arudishiwe karibu Sh6 milioni ambazo alichanga kwa Kanisa Katoliki la Soweto, eneobunge la Embakasi Mashariki mnamo Jumapili.
Pia ameamrisha Sh200,00o ambazo zilitolewa na Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja zirejeshwe akisema kuwa Mswada wa Mchango kwa Umma 2024 unasisitiza kuwa lazima kuwe na idhini kwa asasi ya umma inayolenga kuandaa au kunufaika kupitia mchango unaoshirikisha umma.
Kiongozi huyo wa dini pia alisema kuwa ni kinyume cha kanuni za kanisa hilo kupokea pesa kutoka kwa wanasiasa akisema wanajihadhari na hali ambapo nyumba ya Mungu hutumika na wanaisa vibaya kucheza siasa.
Mnamo Jumapili, Rais Ruto alitoa Sh2 milioni kwa kanisa hilo kujenga nyumba ya padri na akamwomba padri wa kanisa hilo aendee Sh3 milioni nyingine mnamo Jumatatu au Jumanne afisini mwake kukamilisha ujenzi huo.
Pia alitoa Sh600,000 ambapo Sh300,000 zilikuwa zitumike kununulia kwaya ya watoto sare na Sh300,000 nyingine kwa kwaya kuu. Rais pia aliahidi kununulia kanisa hilo basi jipya ambalo alisema atarejea na kuwaletea mnamo Januari mwakani.
Aidha, Gavana Sakaja alitoa Sh200000 kwa kwaya zote mbili, pesa ambazo sasa zitarejeshwa kutokana na agizo la Askofu Anyolo.
“Pesa hizi zitarejeshewa kwa waliozitoa. Wanasiasa wanakaribishwa kanisani ili kulishwa chakula cha kiroho lakini wanashauriwa wafanye hivyo kama waumini wengine,” ikasema sehemu ya taarifa ya Askofu Anyolo.
“Hii itahakikisha kuwa hawatumii nyadhifa zao kwa manufaa ya kisiasa,” ikaongeza taarifa hiyo.
Askofu huyo alirejelea taarifa iliyotolewa na Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki mnamo Ijumaa ambapo walishutumu utawala wa Rais Ruto kama uliojaa uongo na unaohusika na maovu mengi kama ufisadi na utekaji nyara.
Pia walisema utawala huu haujali mahangaiko ya Wakenya kutokana na kuanzishwa kwa Bima ya Afya ya Jamii, ufisadi na pia mfumo mpya wa ufadhili wa elimu kwenye vyuo vikuu ambao umewasababishia wanafunzi mateso mengi.
Alisema dayosisi ya Nairobi inaunga taarifa hiyo na akasisitiza kuwa kanisa siku zote linastahili kutoegemea mrengo wowote wa kisiasa nao viongozi hawafai kutumia vibaya majukwaa kanisani kujipigia debe.