Karibisheni watoto chokoraa wanaorandaranda majumbani mwenu, mke wa Gachagua asihi Wakenya
NA WYCLIFFE NYABERI
MKE wa Naibu Rais Rigathi Gachagua, Dorcas Rigathi, ameyaomba makanisa kuwakumbatia watoto wanaorandaranda mitaani almaarufu kama chokoraa kila mara wanapotaka usaidizi wao.
Bi Rigathi mnamo Jumanne alipeleka injili yake ya kuwatetea watoto wavulana katika Kaunti ya Kisii na kutoa hamasisho kwa wavulana kujikinga dhidi ya matumizi ya dawa za kulevya.
Akionyesha upendo wake kwa watoto wa kurandaranda alipohutubia umati katika uwanja wa Shule ya Msingi ya Kisii, Bi Rigathi aliwasihi wavulana waliojiingiza kwa mihadarati kubadili mienendo yao huku akidokeza kuwa serikali na makanisa, kwa pamoja, wana wajibu wa kutekeleza kuwalinda.
“Kama jamii, serikali na makanisa, tunalo jukumu kuu kuwalinda watoto wa kiume wasiangamie katika uvutaji wa bangi wa dawa nyingine. Nendeni kanisani na nawaomba wachungaji, watoto hawa wanapokuja kwenu, wafungulieni milango na wapeni chakula,” Bi Rigathi alisema.
Mke huyo wa Naibu Rais alisema juhudi za kutosha hazikuwa zimechukuliwa kuwalinda watoto wa kiume kama inavyofanywa kwa wasichana.
Lakini aliahidi kufanya juu chini kubadili hali hiyo, huku alisema atahakikisha waraibu wa pombe watakaotaka kujiunga na shule za kurekebisha unywaji vileo na tabia almaarufu ‘rehabs’ wanasaidika kujiunga na shule hizo.
“Mkikubali kwenda rehab, tutawasaidia tuwezavyo. Mkirekebika pia mnaweza kupewa nafasi kujiunga na vyuo anuwai ili mjiendeleze kimaisha,” Bi Rigathi aliahidi.
Awali, mke wa Naibu Rais alifanya mkutano wa maombi pamoja na wahubiri wa wachungaji kutoka eneo la Kisii.
Aliwaomba watumishi hao wazidi kuliombea taifa la Kenya na hasa Kaunti ya Kisii, ambayo imekuwa ikikumbwa na fujo za malumbano kati ya Gavana wa Kisii Simba Arati na mbunge wa Mugirango Kusini Sylvanus Osoro.
Kufuatia ziara ya Bi Rigathi, wakazi wa Kisii walifaidi na matibabu ya bure.
Viongozi walioandamana naye ni gavana Simba Arati, mbunge wa Nyaribari Chache Zaheer Jhanda na Mwakilishi wa Kike Dorice Aburi.