Karish aidhinishwa kugombea kiti cha Mbeere Kaskazini, asuta wapinzani
WAKAZI wa Mbeere Kaskazini wanajiandaa kwa uchaguzi mdogo wa ubunge baada ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kumuidhinisha rasmi Newton Kariuki, maarufu kwa jina la Karis, kuwania kiti hicho kupitia chama cha Democratic Party (DP).
Kiti hicho kiliachwa wazi kufuatia uteuzi wa aliyekuwa mbunge, Geoffrey Ruku, kuwa Waziri wa Utumishi wa Umma na Rais William Ruto.
Akizungumza baada ya kuidhinishwa na IEBC, Kariuki alielezea imani yake kwamba atawabwaga wapinzani wake licha ya vizingiti alivyokumbana navyo katika harakati za kuwania kiti hicho.
“Nimefurahi kwamba hatimaye nimeidhinishwa kugombea, licha ya majaribio yote ya kunizuia. Maadui walijaribu kunivunja moyo, lakini Mungu ni mkuu,” alisema Kariuki.
Aliandamana na kiongozi wa chama cha DP, Justin Muturi, ambaye alisisitiza kuwa chama chao kiko tayari kwa uchaguzi huo mdogo unaotarajiwa kufanyika mwezi Novemba.
“Hakuna shaka, tutachukua hiki kiti. Lakini tunawasihi wafuasi wetu waendeshe kampeni kwa amani,” alisema Muturi.
Katika uchaguzi huo mdogo, Kariuki atapambana na Duncan Mbui wa chama cha Chama Cha Kazi (CCK) na Leonard Muthende wa United Democratic Alliance (UDA)
Muturi aliwahimiza wafuasi wa DP kujitokeza kwa wingi kupiga kura, akidai kuwa huu ni mwanzo wa kuipinga serikali ya UDA.
“Rais Ruto atakuwa kiongozi wa muhula mmoja tu. Tunawaomba wakazi wa Mbeere wamkatae mgombea wa UDA,” aliongeza Muturi.
Mara baada ya Kariuki kuidhinishwa na IEBC, mamia ya wafuasi wake walimiminika barabarani mjini Siakago kusherehekea tukio hilo kwa nyimbo na ngoma, hali iliyosababisha shughuli za biashara kusimama kwa muda.