Kashfa ya hongo yaibuka TSC walimu wakilia kuuza mali yao ili kupata ajira
KASHFA ya rushwa imeibuka katika Tume ya Huduma ya Walimu (TSC), na kuwaacha walimu waliohitimu wakihangaika licha ya kutoa pesa nyingi wakitarajia kuajiriwa lakini bila mafanikio.
Madai yanahusu kuwepo kwa mtandao wa walaghai katika makao makuu ya TSC, huku maafisa wa kaunti wakitajwa kuwa mawakala, hali inayofichua mfumo ulioota mizizi na ambao ulichochea maandamano katika Kaunti ya Bomet.
Kashfa hiyo ilianza kufichuka wiki iliyopita baada ya waliokata tamaa kuandamana katika eneo bunge la Konoin, Kaunti ya Bomet, wakilaumu maafisa wa TSC kwa kudai hongo ili kuwaajiri.
Walimu wengi wanasema waliuza mali yao, kuchukua mikopo au kutumia akiba yao yote.
Waathiriwa wanadai mara tu pesa zilipolipwa, afisi za TSC katika ngazi ya kaunti zilipokea stakabadhi zao lakini baada ya miezi mitatu hadi mitano, hawajaajiriwa.
Kwa mujibu wa duru zinavyofahamu kinachoendelea katika tume hiyo, mtandao huo unaonekana kuwa umepangwa vizuri.
Maafisa wa kaunti wanadaiwa kuwasaka walimu waliokata tamaa na kuwasilisha pesa wanazopokea, huku maamuzi ya mwisho na utoaji wa barua za ajira ukifanywa katika makao makuu ya TSC.
Kulingana na barua za uhamisho zilizoonekana na Taifa Leo, maafisa wawili wakuu wa TSC katika Kaunti ya Bomet wamehamishwa.
Mkurugenzi wa TSC Kaunti ya Bomet Dkt William Yator, amehamishiwa Kaunti ya Siaya, huku Mkurugenzi wa Kaunti Ndogo ya Konoin, David Kemei, akihamishiwa Kaunti ya Migori.
Akizungumza na Taifa Leo, Kaimu Afisa Mkuu Mtendaji wa TSC, Bi Eveleen Mitei, alisema tume imeunda Kamati Huru ya Uchunguzi kuthibitisha ukweli wa madai hayo.
Tume hiyo ilifichua kuwa tayari imehoji zaidi ya watu 15 kama sehemu ya uchunguzi unaoendelea, ikisisitiza kuwa uhamisho wa maafisa hao ulifanywa ili kuunda mazingira bora ya uchunguzi huru na usio na upendeleo.
“Tume iliunda Kamati Huru ya Uchunguzi kwa mujibu wa Mwongozo ili kufanya uchunguzi wa haki na kubaini ukweli wa madai hayo,” alisema Bi Mitei.
“Tumehamisha Mkurugenzi wa Kaunti ya Bomet na Mkurugenzi wa Kaunti Ndogo ya Konoin mahsusi kuruhusu kamati hiyo kufanya uchunguzi wa kina,” aliongeza.
Tume ilisema Kamati ya Uchunguzi inatarajiwa kukamilisha kazi yake ndani ya siku saba zijazo na kuwasilisha ripoti itakayoongoza hatua zitakazochukuliwa.
“Ninahakikishia umma na wadau wote kuwa tume itachukua hatua kali za kinidhamu dhidi ya afisa yeyote atakayepatikana na hatia kwa mujibu wa mfumo wa kisheria wa tume,” alisema Bi Mitei.