Habari za Kitaifa

Kauli za Raila kuhusu ODM kuweka mgombeaji 2027 zakoroga kambi ya Ruto

Na JUSTUS OCHIENG September 25th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KINARA wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM), Raila Odinga, mnamo Jumatatu alizua mjadala kuhusu siasa za urithi alipofafanua kwamba hakuna kitakachozuia chama hicho kuwania urais katika uchaguzi wa 2027 licha ya handisheki yake ya sasa na Rais William Ruto.

Kauli ya Bw Odinga imeibua wasiwasi katika kambi ya Rais Ruto ambayo ilikuwa ikitegemea pakubwa msaada wa ODM katika kura ya 2027.

“Ni nani alisema ODM haitakuwa na mgombea urais mwaka 2027? Kama ODM tuna mpango wazi ambao tumeelewana na kusaini. (Hata hivyo), maamuzi mengine yatafanywa wakati ukifika,” akatangaza.

Kauli yake ilijiri wiki chache tu baada ya kuambia waombolezaji katika mazishi ya mbunge wa zamani wa Karachuonyo, Phoebe Asiyo, kwamba “mpango wetu wa serikali jumuishi” na Rais Ruto utaendelea hadi 2027.

Kauli ya kiongozi wa ODM imeamsha tena mjadala kuhusu nia yake na kuleta wasiwasi katika Kenya Kwanza.

Katika mazishi hayo mjini Homa Bay mwezi uliopita, matamshi ya Bw Odinga yalifasiriwa kwamba ameamua kugangamala na Rais Ruto.

“Kwa wale wanaosema vingine, tupeni nafasi na mtuhukumu mwaka 2027. Hii (serikali jumuishi) itadumu mpaka 2027; baadaye tutaona tutaenda wapi,” aliambia wakosoaji wa mpango wake na Dkt Ruto.

Maneno hayo yaliwatia moyo wafuasi wake waliokuwa wamejiunga na serikali jumuishi, lakini pia yakaibua malalamishi makali katika baadhi ya mirengo chamani ODM.

Aidha, vinara wa muungano wa upinzani, Kalonzo Musyoka wa Wiper na mwenzake Eugene Wamalwa wa Democratic Action Party–Kenya (DAP-K)walidai kuwa Bw Odinga ameingia rasmi serikalini.

Lakini Jumatano, maafisa wa chama tawala cha United Democratic Alliance (UDA) walielezea hofu kwamba kauli za hivi karibuni za Bw Odinga zinaweza kuvuruga mpango wao wa kisiasa na ODM, japo waliisisitiza kuwa ushirikiano wao bado unazidi kuwa na manufaa kwa pande zote.

Licha ya hayo, ndani ya UDA kuna wazo kwamba wanahitaji mpango mbadala iwapo Bw Odinga atachukua hatua ya kushangaza.

Katibu Mratibu wa Kitaifa wa UDA, Vincent Kawaya, alijaribu kupunguza wasiwasi akisema pande zote zinahitaji kila moja kisiasa kwani ushirikiano wao bado unazidi kuwa na manufaa kwao wote.

“Hakuna lolote baya. Uhusiano wetu na Raila ni ule wa kushirikiana. Tunahitaji kila mmoja na hakuna anayefaa kudhania kuwa Raila hatatuhitaji,” Bw Kawaya alieleza.

Alisema uamuzi wa Bw Odinga kuimarisha ODM ni kwa manufaa ya UDA.

“Kisiasa, njia rahisi ambayo tunaweza kushindwa ni kama ODM haitakuwa imara. Kwa sababu vyama vidogo vinaweza kuibuka na kupenya ngome za Raila. Ni muhimu sana kwetu Raila akiwa na nguvu,” akahoji.

Kulingana naye hakuna makubaliano yoyote yaliafikiwa kuhusu ushirikiano au ugavi wa madaraka baada ya 2027, lakini kudumisha umaarufu wa kisiasa wa Bw Odinga ni muhimu kwa pande zote.

Naibu Katibu Mkuu wa UDA Omboko Milemba alisema mpango wa muungano wao 2027 utaamuliwa na Rais Ruto na Bw Odinga.

“Kuhusu 2027, Raila na Rais Ruto watakubaliana katikma ngazi yao. Tutatekeleza maagizo yao,” alisema.

Seneta wa Nandi Samson Cherargei, mwandani wa Rais Ruto, hata hivyo, alituliza wasiwasi, akisisitiza: “Watu wasijali sana kile Baba Raila Odinga alisema wakati wa mkutano wa wabunge wa ODM, kwa sababu ushirikiano kati ya UDA na ODM unafanya kazi vizuri sana na utaendelea hata baada ya 2027.”

Hata hivyo, Profesa Gitile Naituli wa Chuo Kikuu cha Multimedia anaonya kwamba tabia ya Bw Odinga hufanya iwe vigumu kwake kuunga mkono Dkt Ruto.

“Raila hataki kiongozi wa Luo achukue nafasi yake wakati bado yupo hai. ODM itaweka mgombea wa urais, na kuna uwezekano mkubwa kuwa ni Raila mwenyewe,” Prof Naituli alisema.