• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 7:12 PM
Kaunti kutia mfukoni Sh35 bilioni kila mwaka

Kaunti kutia mfukoni Sh35 bilioni kila mwaka

NA ERIC MATARA

KAUNTI 21 zinamezea mate mapato ya zaidi ya Sh35 bilioni kila mwaka katika mpango wa Rais William Ruto wa kugawana 50:50 mapato ya mbuga za kitaifa za wanyamapori kati ya serikali ya kitaifa na serikali za kaunti.

Agosti iliyopita, Rais Ruto alikubali shinikizo kutoka kwa kaunti zilizotaka sehemu ya mapato yanayotokana na mbuga za kitaifa za wanyamapori kugawiwa kaunti baada ya kuagiza viwango viwili vya serikali kugawana hela kwa usawa.

Baadhi ya kaunti zinazotazamiwa kunufaika kutokana na agizo hilo la Rais kuhusu kugawana mapato ni pamoja na; Nakuru, Nairobi, Samburu, Baringo, Narok, Laikipia, Taita Taveta, Nyeri, Turkana na Trans Nzoia.

Kaunti nyinginezo ni Homabay, Machakos, Kisumu, Meru, Bungoma, Marsabit, Tana River, Makueni and Nyandarua.

Serikali za kaunti kwa miaka mingi zimekuwa zikishinikiza kugawiwa sehemu ya mapato yanayotokana na mbuga za kitaifa za wanyamapori.

Hela hizo zinatazamiwa kupiga jeki vituo vya mapato ya kaunti binafsi.

Hata hivyo, Taifa Dijitali ilibaini Jumatatu, Aprili 1, 2024 kuwa miezi saba baada ya agizo la Rais, kaunti bado hazijapokea mapato hayo huku magavana wakizidisha shinikizo kwa serikali ya kitaifa kufanya hima kuhusu mpango huo.

“Nairai Wizara ya Utalii na Wanyamapori kuwezesha kusambazwa kwa mapato yanayotokana na mbuga kwa kaunti kwa kuambatana na agizo la Rais mwaka jana (2023). Natoa wito vilevile kwa Wizara na Shirika la Wanyamapori Nchini (KWS), kuangazia suala la visa vya mara kwa mara vya wanyamapori kushambulia binadamu katika Kaunti ya Kwale,” alisema Gavana Fatuma Achani.

Wengine wanaotaka agizo hilo litekelezwe upesi wanajumuisha Gavana wa Taita-Taveta, Andrew Mwadime na wenzake Joseph Ole Lenku (Kajiado) na Susan Kihika (Nakuru).

Hata hivyo, duru zimefichua kuwa Wizara na KWS zimeanzisha mchakato kubuni mbinu na mfumo wa kisheria kuhusu utekelezaji wa sheria hiyo.

 

  • Tags

You can share this post!

Nusra Man City imuue Ndovu ikimshusha juu ya mti

Wakenya wachongoana mitandaoni wakisherehekea ‘April...

T L