Habari za Kitaifa

Kaunti tajiri zashindwa sasa kulipa madeni yao

February 25th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA BRIAN AMBANI

KAUNTI za Kiambu, Nairobi, Narok na Kajiado ni miongoni mwa kaunti tajiri zinazotumia pesa chache zaidi kulipa madeni wanayodaiwa na watoaji huduma na bidhaa.

Kiambu imelipa asilimia nne pekee ya madeni, na kuifanya kuwa kaunti mbaya zaidi nchini kuuzia bidhaa na huduma.

Takwimu kutoka kwa Wizara ya Fedha zinaonyesha Kiambu ilikuwa na madeni ya Sh3.36 bilioni kufikia Aprili 2023 lakini ikalipa Sh143.3 milioni pekee.

Katika mwaka huu wa fedha unaoisha Juni, kaunti hiyo ilitengewa Sh12.22 bilioni.

Nairobi imelipa asilimia tisa pekee ya madeni ya Sh10.6 bilioni.

Kaunti hiyo imelipa Sh975.2 milioni pekee, licha ya kutengewa Sh20 bilioni katika mgao wa kitaifa.

Kaunti tatu – Nyeri, Siaya na Mandera – zimelipa madeni yote.

Mandera imelipa madeni ya Sh195.6 milioni, Siaya Sh239.4 milioni na Nyeri Sh47 milioni.

Kaunti ambazo zimelipa sehemu kubwa zaidi ya madeni ni Murang’a (asilimia 99.7), Lamu (asilimia 99), Nyamira (asilimia 99), Migori (asilimia 96) na Samburu (asilimia 95).