Habari za Kitaifa

Kaunti tano zaibuka mfano bora katika matumizi ya pesa kwenye maendeleo

Na ERIC MATARA July 8th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

KAUNTI tano zilitumia jumla ya Sh10 bilioni katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika miezi tisa ya kwanza katika mwaka wa fedha wa 2023/2024.

Kulingana na ripoti ya Utekelezaji wa Bajeti katika Kaunti ya kipindi hicho iliyotolewa na Msimamizi wa Bajeti Margaret Nyakang’o kaunti hizo tano ni; Narok, Bomet, Uasin Gishu, Mandera na Kitui.

Kaunti hizi zilitumia mgao wa fedha za maendeleo kwa kima cha asilimia 54.4 per cent, asilimia 48.8, asilimia 41.5, asilimia 38 na asilimia 36.6, mtawalia.

Miongoni mwa kaunti hizo, kaunti ya Narok ndio iliongoza katika matumizi ya fedha za maendeleo kwa kuandikisha kiwango cha asilimia 54.4.

Kiwango hicho kinazidi, kima cha matumizi ya fedha za maendeleo katika jumla ya kaunti 10.

“Serikali zote za kaunti zilitumia Sh44.89 bilioni katika shughuli za maendeleo, sawa na asilimia 22.1 ya mgao wa bajeti ya maendeleo ya Sh203.48 bilioni kwa mwaka katika kaunti zote 47,” ripoti hiyo inasema.

Ripoti hiyo inaeleza kuwa kaunti ya Narok ilitumia Sh2.9 bilioni kwa maendeleo, Mandera ilitumia (Sh1.9 bilioni), Kitui (Sh1.8 bilion), Uasin Gishu (Sh1.68 bilioni) na Bomet (Sh1.16 bilioni).

Ni kaunti hizo tano ziliibuka kutumia pesa nyingi katika maendeleo, kwa kutumia zaidi Sh1 bilioni ndani ya kipindi hicho kilichofanyiwa uchunguzi.

Dkt Nyakang’o pia alifichua jinsi kaunti zingine 42 zilifeli kutumia fedha zilizotengewa miradi ya maendeleo.

Aidha, ripoti hiyo inaonyesha kwamba kaunti za Nairobi, Bungoma, Mombasa na Taita Taveta ndizo zilitumia kiasi kidogo zaidi za fedha za bajeti za maendeleo.