• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Kaunti zamegewa mgao kidogo

Kaunti zamegewa mgao kidogo

NA CHARLES WASONGA

SERIKALI za kaunti zimepata pigo baada ya kutengewa Sh391 bilioni katika mwaka wa kifedha wa 2024/2025 badala ya mgao wa Sh450 bilioni ambazo magavana waliitisha.

Kwa upande mwingine, Serikali ya Kitaifa imetengewa Sh2.5 trilioni za mapato ya serikali katika mwaka huo wa kifedha unaoanza Julai 1, 2024.

Aidha, kulingana na Mswada wa Ugavi wa Mapato wa 2024 uliowasilishwa katika Bunge la Kitaifa na mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti Ndindi Nyoro mnamo Jumatano, Hazina ya Usawazishaji Kimaendeleo imetengewa Sh7.8 bilioni.

Baraza la Magavana (CoG) limekuwa likishikilia kuwa serikali 47 za kaunti zitengewe Sh450 kama mgao wa kifedha kutoka kwa bajeti ya Sh470 bilioni lililopendekeza awali.

Aidha, Tume ya Ugavi wa Mapato (CRA) ilikuwa imependekeza kuwa serikali za kaunti zitengewe Sh407 bilioni badala ya Sh416 bilioni.

Bw Nyoro ambaye pia ni Mbunge wa Kiharu, alisema kuwa Sh399 bilioni ambazo zitatengewa serikali za kaunti zinawakilisha ongezeko la Sh16.6 bilioni kutoka kwa mgao wa mwaka uliopita wa kifedha.

“Magavana hawafai kulalamika kwa sababu Sh391 bilioni ni sawa na asilimia 24.9 ya mapato ya serikali yaliyofanyiwa ukaguzi. Serikali inakabiliwa na changamoto za kifedha kutokana na ugumu wa kupata fedha katika masoko ya humu nchini na yale ya kimataifa,” akasema Bw Nyoro.

Wiki jana, mwenyekiti wa CoG Anne Waiguru alifika mbele ya Kamati ya Seneti kuhusu Fedha na kulalamikia mwenendo wa serikali kuendelea kukwamilia fedha zinazofaa kuelekezwa kwa serikali za kaunti.

Bi Waiguru ambaye ni Gavana wa Kirinyaga alilalamika kuwa baadhi ya serikali za kaunti hazijalipa mishahara ya wafanyakazi kufuatia kucheleweshwa kwa usambazaji wa fedha kutoka kwa Hazina ya Kitaifa.

“Baadhi ya kaunti zimelazimika kuchukua mikopo ya riba ya juu ili kulipa wafanyakazi,” akaeleza Bi Waiguru.

  • Tags

You can share this post!

Jinsi nyama ya kasa inavyotayarishwa kuepuka vifo kama...

Kang’ethe anayedaiwa kuua mpenziwe ‘majuu’ alia...

T L