Habari za Kitaifa

Kaunti zaongezewa bilioni saba juu na kuambiwa ziache kulialia

Na WAANDISHI WETU November 21st, 2024 Kusoma ni dakika: 2

SERIKALI za kaunti zitapokea Sh387 bilioni kama mgao wa mapato ya kitaifa baada ya Kamati ya Upatanishi inayojumuisha wanachama wa Bunge la Kitaifa na Seneti kuafikiana kuhusu Mswada uliokwama wa Mgao wa Mapato, 2024.

Kikosi cha Upatanishi kilimaliza mzozo ambao ulitishia kulemaza huduma katika kaunti 47 baada ya Bunge la Kitaifa kubatilisha pendekezo la Sh400 bilioni ambazo kaunti zilikuwa zimetengewa katika Mswada wa awali wa mgao wa Mapato, 2024.

Bunge la Kitaifa lilikuwa limepunguza mgao wa mapato kwa kaunti kwa Sh20 bilioni kutoka Sh400 bilioni hadi Sh380 bilioni kufuatia kukataliwa kwa Mswada wa Fedha wa 2024.

“Tumekubali kutengea kaunti Sh387 bilioni zikijumuisha Sh385 bilioni ambazo zilitengwa katika mwaka wa kifedha wa 2023/24 na Sh2 bilioni za ziada ili kukidhi shinikizo la mfumuko,’’ Ndindi Nyoro, mwenyekiti mwenza wa Kamati ya Upatanishi.

Makubaliano hayo yamefikiwa siku moja baada ya Waziri wa Fedha John Mbadi kuwataka magavana kukubali mgao wa Sh380 bilioni katika mwaka huu wa kifedha wa 2024/2025.

Kuongeza kiwango mwaka ujao

“Magavana wanafaa kukubali Sh380 bilioni pekee katika mwaka huu wa kifedha huku tukitafuta njia za kuongeza kiwango hicho mwaka ujao,” akasema.

“Ningependa kuzipa serikali za kaunti pesa zaidi lakini nimebanwa, uchumi wetu hauwezi kufadhili hatua hiyo wakati huu,” Bw Mbadi akasema Jumanne kwenye mahojiano na Taifa Leo kwa njia ya simu.

Mbunge huyo wa zamani wa Suba Kusini alisema haitakuwa na maana yoyote kwa Hazina ya Kitaifa kuahidi mgao wa Sh400 bilioni kwenye karatasi kisha ifeli kutoa pesa hizo na kupelekea deni kubwa ambalo serikali za kaunti zitakuwa zikidai serikali kuu.

Bw Mbadi alionekana kukaidi msimamo wa kiongozi wa chama chake cha ODM Raila Odinga aliyeunga mkono msimamo wa maseneta na magavana kwamba, serikali za kaunti zitengewe Sh400.1 bilioni.

Kwenye kikao na wanahabari katika afisi zake zilizoko jumba la Capitol Hill Nairobi, Bw Odinga aliwasuta wabunge waliopendekeza mgao wa Sh380 bilioni akidai wanahujumu ugatuzi.

Kupigania katiba ya sasa

Bw Odinga, ambaye ni mmoja wa viongozi waliopigania kupatikana kwa Katiba ya sasa, alisema mgao huo uliopendekezwa na wabunge haufikii kiwango kinachokubalika na Katiba inayosema kuwa kaunti zitengewe angalau asilimia 15 ya mapato ya serikali.

“Mvutano ulioko sasa na jaribio la kupunguza mgao wa fedha kwa kaunti ni hatari na linaturudisha nyuma. Nawaomba wabunge waunge ugatuzi unawiri na wasionekane kuwa washirika wa watu wenye nia ya kuua,” Bw Odinga akawaambia wanahabari.

Mnamo Jumanne, magavana walitishia kusitisha shughuli baada ya siku 30 iwapo wabunge na maseneta hawangeelewana kuhusu kiasi cha fedha kinachofaa kutengewa kaunti.

Akizungumza baada ya kuongoza mkutano maalum wa Baraza la Magavana (COG) jijini Nairobi, Mwenyekiti Ahmed Abdullahi alisema, walikasirishwa na Bunge la Kitaifa kusisitiza kaunti zingepata Sh380 bilioni, na si Sh400 bilioni kama ilivyopendekezwa na Seneti.

Uhaba wa fedha

Gavana Abdullahi alisema licha ya kaunti kuathiriwa na uhaba wa fedha, serikali ya kitaifa iliendelea kupokea mgao wake baada ya Bunge la Kitaifa kupitisha Sheria ya Matumizi ya Ziada ya 2024.

Kwa kutokuwa na Sheria ya Ugavi wa Mapato kwa Kaunti, serikali za kaunti zinapaswa kupokea hadi asilimia 50 ya mapato sawa kutokana na bajeti ya mwaka wa kifedha wa 2023/2025.

Mnamo Jumanne, magavana walifokea Bw Mbadi kwa kudai alikuwa ametoa pesa kwa kaunti kufikia Oktoba 2024.

Gavana wa Kakamega Fernades Barasa alikanusha madai hayo na kusisitiza kaunti zinakabiliwa na uhaba mkubwa wa fedha na kufikia Januari, shughuli zote zingekwama iwapo wabunge na maseneta hawangefikia muafaka.

RIPOTI ZA EDWIN MUTAI, CHARLES WASONGA na BENSON MATHEKA