Habari za Kitaifa

Kaunti zinavyoporwa kwa kukosa sajili za mali

March 12th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA ERIC MATARA.

SERIKALI nyingi za kaunti zimepoteza mali ya thamani ya mabilioni ya pesa ndani ya miaka 12 iliyopita kutokana na ukosefu wa sajili halali za mali zao.

Hali hiyo imeacha mali hizo katika hatari ya kuporwa.

Mfumo wa ugatuzi ulipoanza 2013, serikali za kaunti zilipasa kuandaa na kuhifadhi sajili za mali ziliyopasa kuwasilisha kwa Kamati ya Kiufundi ya Serikali Kuu na Serikali za Kaunti (IGRTC)

Hata hivyo, Taifa Leo Dijitali imebaini kuwa tangu wakati huo nyingi za serikali za kaunti hazina sajili sahihi za mali zao; zilizorithi kutoka kwa mabaraza ya miji na manispaa.

Kaguzi nyingi zilizoendeshwa na Afisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali zimefichua kwamba mali ambazo huenda ziliporwa ni pamoja na majengo, ardhi, mitambo ya ujenzi wa barabara, magari, vifaa vya afisi, fanicha, vifaa vya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT), maeneo ya turathi na utamaduni miongoni mwa nyingine.

Ripoti kadha za ukaguzi zinaonyesha kuwa miongoni mwa kaunti ambazo huenda mali zao ziliporwa kwa ukosefu wa sajili sahihi ni pamoja na Nakuru, Kericho, Nairobi, Trans Nzoia, Uasin Gishu, Bomet, Mombasa, Kisii, Nyamira, Elgeyo Marakwet, Migori miongoni mwa zingine.

Kutokuwepo kwa sajili za mali kunaashiria uwezekano wa kupotea kwa mali kwa kutwaliwa na watu binafsi.

Taarifa iliyotolewa juzi na Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) iliibua hofu kuhusu mfumo mbaya wa uwekaji na usimamizi rekodi katika kaunti zote 47, zikiwemo sajili za mali.

Tume hiyo ilisema hali hiyo hutoa mwanya kwa ufisadi na hatari ya kupotea kwa mali ya umma.

Kupitia barua iliyotuma kwa serikali hizo za kaunti, EACC imewataka maafisa wakuu wa kaunti hizo na mabunge ya kaunti kuanzisha mageuzi ya haraka ya usimamizi wa rekodi ili kuziba mianya ya ufisadi.

Kulingana na afisa mkuu mtendaji wa tume hiyo Twalibu Mbarak, uchunguzi wao ulibaini dosari nyingi katika usimamizi wa rekodi katika serikali za kaunti na mabunge ya kaunti.

“EACC imegundua kuwa Sajili za Mali ambazo ni sahihi hazijahifadhiwa. Serikali nyingi za kaunti ziko na sajili za mali ambazo hazina maelezo muhimu kama vile nambari za mpangilio (serial numbers), ukadiriaji wa thamani na mahala ziliko mali hizo. Mali hazina nambari za utambulisho ili ziweze kutambuliwa kwa urahisi ili kuimarisha uwajibikaji,” EACC ikaeleza.

Tume hiyo ilisema stakabadhi za umiliki wa baadhi ya mali kama vile ardhi, mashine, vifaa na magari zinaonyesha kuwa mali hizo zingali zimesajiliwa kwa majina ya mabaraza ya wilaya.

EACC inasema hali kama hii nyakati zingine zimechangia kunyakuliwa, kuingiliwa na kuibiwa kwa mali hizo.

Tume hiyo pia ilisema kuwa Kamati za Kuuza Mali hazijabuniwa katika baadhi ya kaunti ili kutoa mwongozo kuhusu uuzaji wa mali kuukuu, zilizopitwa na wakati au zisizoweza kutumika.