Kaunti zinavyotumia mawakili kutafuna pesa za umma
BODI ya Utumishi wa Umma ya Kaunti ya Marsabit ilikodi huduma za mawakili kwa gharama ya Sh10.3 milioni kuitetea katika kesi ambapo ilishtakiwa kwa kuzuiliwa gari la mlalamishi mmoja, ripoti ya ukaguzi imefichua.
Mlalamishi huyo alitaka alipwe Sh1 milioni kama hasara kutokana na kuharibika kwa gari hilo.
Ripoti hiyo ya Mkaguzi wa Hesabu za Serikali Nancy Gathungu kwa mwaka wa kifedha uliokamilika Juni 30, 2024 ilifichua kuwa hakukuwa na ushahidi kwamba ada hiyo ilikadiriwa kwa kuzingatia viwango vya malipo kwa mawakili.
Hata hivyo, katika Kaunti ya Marsabit hali ilikuwa ya kipekee kwani mawakili walilipwa mamilioni ya fedha, ambao waliteuliwa kwa njia inayokiuka sheria.
Kaunti ya Nairobi imekuwa ikigonga vichwa vya habari kwa kulipa viwango vya juu kupitia ada za mawakili.
Ni kutokana na hali hiyo ambapo serikali hiyo inayoongozwa na Gavana Johnson Sakaja anadaiwa Sh6.26 bilioni na mawakili, kiasi kinachowakilisha asilimia 29 ya Sh21.37 bilioni ambazo ni madeni ya ada za mawakili.
Isitoshe, deni la malipo ya ada ya mawakili linawakilisha asilimia 11 ya madeni yote ambayo hayajalipwa na serikali ya Kaunti ya Nairobi.
Serikali ya kaunti hiyo inapambana na jumla ya kesi 1,086 zinazotokana na madai yaliyowasilishwa dhidi yake kufuatia utendakazi wake.
“Ikiwa pesa hizo zote ambazo serikali ya Kaunti ya Nairobi inadaiwa zitalipwa, hiyo itaathiri uwezo wake wa kutoa huduma,” inasema ripoti hiyo ya Bi Gathungu.
“Ilibainika kuwa kesi nyingi zilihusu masuala kama kutolipiwa kwa bidhaa, kazi au huduma zilizotolewa na wanakandarasi mbalimbali, kukatizwa kwa kandarasi kinyume cha sheria, ukiukaji wa sheria katika utoaji wa zabuni na usimamizi mbaya wa kandarasi,” ripoti hiyo inaongeza.
Ripoti hiyo ya mkaguzi wa hesabu za serikali pia iligundua kuwa mawakili walikuwa wakiteuliwa bila ushindani wowote inavyohitajika kisheria.
“Kutokuwepo kwa ushindani katika utaratibu wa uteuzi wa mawakili kulichangia kuongezwa kwa gharama ya huduma hizo na ukosefu wa nafasi ya kuwapata mawakili waliohitimu zaidi,” ripoti hiyo inaongeza.
Kwa upande wake, serikali ya Kaunti ya Narok ililipa Sh364.9 milioni kama ada za mawakili ikivuka bajeti ya ukodishaji wa huduma ya Sh337.3 milioni.
Kaunti ya Kajiado nayo ilitumia Sh79. 1 milioni kulipia ada za mawakili ambao walipewa kandarasi hizo pasi na sheria kuzingatiwa.
Serikali ya Kaunti ya Siaya inayoongozwa na Gavana James Orengo, ililipa Sh34.6 milioni kama ada za mawakili.
Kati ya pesa hizi, Sh26 milioni zililipwa kampuni moja ya mawakili na hakukuwa na stakabadhi za kuonyesha kuwa malipo hayo yalitolewa.
Nayo Kaunti ya Mombasa ilitumia Sh67.5 milioni kulipa ada za mawakili walioiwakilisha katika kesi mbalimbali mahakamani.
Kilifi nayo ililipa Sh71.57 milioni kwa mawakili sita na washauri wa kisheria bila stakabadhi za malipo kuonekana na wakaguzi au idhini kutoka kwa afisi ya Gavana.
Kaunti ya Tana River, chini ya Gavana Dhadho Godhana, nayo ililipa kampuni nne za mawakili Sh30.7 milioni kinyume cha sheria huku ile ya Mandera ikitumia Sh45.5 milioni kugharamia ada ya mawakili bila kuidhinishwa na asasi za kisheria.
Kaunti ya Machakosa ililipa Sh38.8 milioni kwa kampuni nne za mawakili huku, Kiambu ikilipa jumla ya Sh517.3 milioni.
Kaunti ya Turkana ililipa Sh165.6 milioni kama ada za mawakili kuhusiana na kesi 14 katika mahakama mbalimbali huku ikitoa zabuni ya kuendesha kesi 24 kwa kampuni saba za mawakili.
Uasin Gishu nayo ilitumia Sh25.5 milioni kukodisha huduma za mawakili ilhali ina afisi ya mwanasheria mkuu yenye mawakili kadhaa.
Kwa upande wa serikali ya Kaunti ya Nandi inayosimamiwa na Gavana Stephen Sang, ilitumia Sh36.8 milioni kukodi huduma za mawakili huku ile ya Vihiga ikitumia Sh71.45 milioni.
Serikali ya Kaunti ya Busia chini ya Gavana Paul Otuoma, ilitumia Sh8.5 milioni kukodi huduma za mawakili wa kibinafsi nayo Kisumu inayoongozwa na Profesa Peter Anyang Nyong’o ikitumia Sh46 milioni.
Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Bi Gathungu pia aliibua maswali kuhusu matumizi ya Sh11 milioni, pesa za umma kukodi huduma za mawili kuiwakilisha serikali ya Kaunti ya Homa Bay katika kesi 350.
Nayo Migori inayoongozwa na Ochilo Ayacko ilitumia Sh50.3 milion, Kisii ikitumia Sh15 milioni na Elgeyo Marakwet ikitumia Sh2.7 milioni bila idhini ya serikali kukodisha huduma za mawakili.