Kawira alaumu Ruto kwa masaibu yake
ALIYEKUWA Gavana wa Meru, Kawira Mwangaza, ameapa kupinga kuondolewa kwake ofisini hadi mahakama ya juu zaidi ili kusafisha jina lake.
Akitaja kufutwa kwake kama dhuluma kubwa iliyoendeshwa na mfumo usio wa haki, Bi Mwangaza pia ameahidi atakabiliana kisiasa na wapinzani wake.
Katika kile kilichoonekana kama mashambulizi kwa Idara ya Mahakama na Rais William Ruto, alidai kuwa serikali ya kitaifa ilikuwa na mkono katika suala hilo, huku pia akilaumu mfumo wa ukandamizaji wa wanawake na wapinzani wa kisiasa kwa masaibu yake.
Bi Zipporah Kinya, aliyewasilisha hoja ya kumwondoa Mwangaza, ni Mwakilishi Wadi aliyeteuliwa Na chama cha UDA huku hoja ya pili ikiwasilishwa na Evans Mawira, aliyekuwa kiongozi wa wengi wa UDA mwaka wa 2023 kabla ya kuhamia kambi ya Mwangaza na kupokonywa wadhifa wake.
Mwangaza alisema kwamba waliompiga vita walifichua waziwazi mchango wao wakati wa kuapishwa kwa gavana mpya, Isaac Mutuma.
“Baadhi yao hata walishukuru uongozi wa juu wa nchi kwa msaada waliopata kufanikisha mpango wao,” alisema.
Alidai kuwa badala ya serikali kuu kuheshimu utawala wa sheria, ilihusika moja kwa moja katika kuhakikisha kuwa sauti za wakazi wa Meru waliomchagua zilipuuzwa.
“Hata mahakama, ambayo ingepaswa kuwa kimbilio langu, ilitumiwa ili kunizuia kupata haki. Huu sio tu unyanyasaji dhidi yangu, bali ni shambulizi kwa demokrasia, usawa wa kijinsia, na haki za kila mwanamke wa Kenya anayetaka uongozi,” alisema.
Akizungumza kwa mara ya kwanza tangu alipopoteza wadhifa wake, Mwangaza alidai kuwa aligeuzwa kuwa ‘kafara ya kisiasa’ ili kupunguza msukosuko wa kisiasa katika Kaunti ya Meru.
“Sitanyamazishwa. Nitatumia hatua zote za kisheria kusafisha jina langu na kufichua dhuluma zilizofanywa dhidi yangu. Haya sio tu mapambano yangu binafsi, bali ni vita kwa kila mwanamke anayetamani uongozi katika jamii ambayo mara nyingi inajaribu kuzima ndoto zao,” alisema.
Mwangaza, ambaye aling’olewa rasmi wiki iliyopita baada ya Mahakama Kuu kuthibitisha uamuzi wa Seneti, aliahidi kuendelea na mapambano ya kisiasa kaunti ya Meru.
Alitangaza mpango wa kuzindua chama cha kisiasa, huku akionyesha matumaini ya kurejea kwenye kinyang’anyiro cha ugavana mwaka wa 2027.
“Kuondolewa kwangu kumenifunza kuwa si busara kuwania ugavana bila chama cha kisiasa. Kuanzia sasa, nitazidisha mikutano ya kisiasa Meru kutambua viongozi wa kushirikiana nao mwaka wa 2027. Pia nitaendelea na shughuli zangu za kusaidia jamii,” alisema.
Mwangaza, ambaye bado anapinga uamuzi wa kumwondoa afisini katika Mahakama ya Rufaa, aliahidi kuwa atakuwa akipiga darubini utawala mpya wa kaunti hiyo.
“Natoa wito kwa Wakenya wote, mashirika ya kijamii, na jamii ya kimataifa kusimama nami kulaani unyanyasaji huu wa mamlaka na kudai uwajibikaji kutoka kwa waliohujumu demokrasia yetu,” alisisitiza.
Alidai kuwa aliondolewa kwa sababu alikataa kutii shinikizo za kisiasa kutoka kwa wanasiasa waliotaka kutumia ofisi yake kwa maslahi yao binafsi.
“Utawala wangu ulitanguliza maslahi ya wananchi kwa kuleta maendeleo makubwa katika sekta ya afya, elimu, miundombinu, na kilimo,” alisema.
Alisema haogopi vitisho vya kuchunguzwa kwa ufisadi.
“Kuna watu wananiambia kuwa nitachunguzwa na DCI na EACC. Sihofii uchunguzi. Nimepata mali yangu kupitia biashara tangu nikiwa msichana mdogo. Nilifanya kazi kama mfanyakazi wa nyumbani, mjakazi, muuzaji wa makaa na mboga, na hata nikawa dereva wa matatu,” alisema.
Aliukosoa utawala mpya wa kaunti, akidai kuwa hauwezi kutumikia maslahi ya wananchi bali wale walio na nia ya ufisadi.
Gavana mpya wa Meru, Isaac Mutuma, alianza kazi yake rasmi kwa kukutana na mawaziri wa kaunti, maafisa wakuu wa idara, na wakuu wa vitengo mbalimbali vya kaunti.
Mutuma aliahidi kuleta maendeleo kwa kushirikiana na wadau wote.
Pia, aliahidi kuboresha hali ya wafanyakazi wa kaunti ambao alisema wameteseka kwa miaka miwili.