Habari za Kitaifa

Kazeni mishipi, itachukua miaka mitatu uchumi kuimarika, asema Kindiki

Na  PIUS MAUNDU December 2nd, 2024 Kusoma ni dakika: 2

WAKENYA wanapaswa kujiandaa kwa nyakati ngumu za kiuchumi, Naibu Rais Kithure Kindiki amesema huku akitoa wito wa uvumilivu serikali inapoweka mikakati ya kuinua mapato ya familia nchini.

Akizungumza baada ya ibada ya Jumapili eneo la Kyuso katika Kaunti ya Kitui, Profesa Kindiki alikadiria kuwa itachukua utawala wa Rais William Ruto angalau miaka mitatu kuimarisha uchumi.

“Kupitia bidii na neema ya Mwenyezi Mungu, tumeweza kuleta utulivu wa viashiria vya uchumi mkuu wa nchi yetu katika miaka miwili iliyopita. Hizi ni fedha za kigeni, bei ya mafuta na bidhaa muhimu kama unga na sukari, na mfumuko wa bei,” alisema.

Akaongeza: “Tunajua bado hatujafika. Bado kuna kazi kubwa ambayo inahitaji kufanywa ili kuleta utulivu wa uchumi. Kwa kuwa viashiria vya uchumi mkuu vimetulia, kazi iliyosalia katika miaka miwili, mitatu ijayo kabla ya sisi kwenda kwa uchaguzi ni kuwawezesha raia kuwa na pesa zaidi mifukoni mwao,” Prof Kindiki aliwaambia washariki katika Kanisa la Kyuso Gospel Outreach Church.

Kama sehemu ya hatua ambazo serikali imeweka ili kuimarisha uchumi na hatimaye kuweka pesa mifukoni mwa Wakenya, Prof Kindiki aliorodhesha mpango wa ujenzi wa nyumba za bei nafuu ambao alisema ulibuniwa kuunda nafasi za kazi na kuchochea biashara katika tasnia ya utengenezaji bidhaa.

Vituo vya ICT kote nchini kuunda nafasi za kazi za kidijitali, na uhamiaji wa wafanyikazi ambao umewafanya vijana kujipanga kupata nafasi za kazi zenye ujuzi na usiokuwa za ujuzi katika nchi za kigeni.

“Kwa sasa tunashughulika na viashiria vya uchumi mdogo. Hizi ni kuunda ajira na mapato ya familia. Ninataka kuwahakikishia Wakenya wote kwamba katika miaka mitatu ijayo, viashirio vyetu vya uchumi mdogo vitakuwa vimetulia na kuwa bora kwa sababu sehemu ngumu ya safari ya kufufua uchumi tayari imeshughulikiwa. Kwa mara ya kwanza Kenya haitaagiza kutoka nje mahindi na sukari. Tunashukuru  kwa hali nzuri ya hewa na mpango wa ruzuku ya mbolea na sera nzuri ambazo serikali hii imeweka,” Prof Kindiki alisema.

Siasa zilitawala ibada ya Jumapili ambayo pia ilihudhuriwa na Seneta wa Tharaka Nithi Mwenda Gataya, Mwakilishi wa Wanawake wa Trans Nzoia Lilian Siyoi, na wabunge Eric Wamumbi (Mathira), Patrick Munene (Chuka Igambang’ombe), Bernard Kitur (Nandi Hills), Nimrod Mbai (Kitui Mashariki) na Paul Nzengu (Mwingi Kaskazini).

Naibu Rais pia alimkemea Bw Gachagua kuhusu msukumo wake wa kuadhibu kaunti ambazo hazikumuunga mkono Rais Ruto katika Uchaguzi Mkuu wa 2022 akitaka zibaguliwe wakati kwa miradi mikubwa na nyadhifa za serikali.

IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA