Habari za Kitaifa

KCSE 2024: Watahiniwa 840 kukosa matokeo, wengine 2,891 wakichunguzwa

Na CHARLES WASONGA January 9th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

MATOKEO ya watahiniwa 840 waliofanya mtihani wa kitaifa wa kidato cha nne (KCSE) mwaka uliopita, 2024, yamefutuliwa mbali kwa kubainika walishiriki udanganyifu.

Akitoa matokea ya mtihani huo Alhamisi, Januari 9, 2024, Waziri wa Elimu Julius Migos Ogamba alisema matokeo ya jumla ya watahiniwa 2, 829 bado yanachunguzwa ndani ya siku 20 kubaini ikiwa walishiriki uovu huo au la.

“Jumla ya watahiniwa 840 wa KCSE ya mwaka jana hawatapata matokeo yao kwani yamefutiliwa mbali ilipobainika kuwa walihusika katika visa vya udanganyifu. Aidha, baraza la kitaifa la mitihani (KCSE) linachunguza matokeo ya watahiniwa 2, 8291 kubaini ikiwa walishiriki udanganyifu au la,” Bw Ogamba akaeleza.

“Uchunguzi huo utaendelea kwa muda wa siku 20 zijazo,” Waziri akaongeza.

Aidha, Bw Ogamba alifichua kuwa ilibainika wataalamu 91 walisaidia au kufanikisha udanganyifu katika KCSE 2024.

Ufichuzi wa Waziri Ogamba kuhusu visa vya udanganyifu katika mtihani wa KCSE 2024, ni kinyume na msimamo wa KNEC na Wizara ya Elimu kipindi cha mtihani mwaka jana, kwamba hakukuwa na visa vyovyote vya udanganyifu.