KCSE: Tovuti ya Knec yagoma maelfu ya watahiniwa wakitafuta matokeo
UPDATE: Tovuti ilirejea sawa 11:40 am -Mhariri
NA MWANGI MUIRURI
Msongamano mkubwa umekumba tovuti ya tume ya mitihani nchini (KNEC) baada ya serikali kuzima huduma ya jumbe za simu ambayo imekuwa ikitumika hapo awali.
Hi ni baada ya jumbe hizo za simu kushukiwa kukosa uadilifu na pia baadhi ya wanasiasa kuhoji njia ambazo zimekuwa zikitumika kutoa kandarasi.
Badala yake, serikali mnamo Januari 8, 2024 kupitia Waziri wa Elimu Bw Ezekiel Machogu ilitangaza https://results.knec.ac.ke kama tovuti mbadala ya kujipatia matokeo.
Walimu, wanafunzi na wazazi walielezea matatizo na mahangaiko wakijaribu kufikia matokeo hayo, wahandisi wa kimitambo katika KNEC wakisema shida ni msongamano.
“Kwa dakika moja tangu tufungue tovuti hiyo baada ya kuipakia matokeo tunapata zaidi ya watumizi 350,000. Hilo ni janga kwa intaneti na miundombinu hapa. Tutazidi kuimarisha hali na pia kudhibiti ustadi wa miale yetu ndio kasi ya huduma ibakie imara,” akasema Bw James Gitau, mhandisi wa kimitambo katika wizara.
Alisema kwamba kufikia saa tano asubuhi, matokeo 1,200 yalikuwa yamepeperushwa kwa waliotuma maombi huku kukiwa na watahiniwa 899, 453.
Hata hivyo, alisema kwamba wageni wanaotarajiwa katika tovuti hiyo ni zaidi ya 3.5 milioni.
“Hali hii inatokana na wengine kando na wanafunzi, wazazi na walimu ambao watakuwa wakitembelea tovuti hiyo kama watalii lakini kwa kuwa watahitaji nambari ya usajili wa mtihani kupenya, hawatafikia matokeo licha ya kuchangia msongamano,” akasema.
Aliongeza kwamba tovuti hiyo imekingwa dhidi ya wadukuzi.