Kenya hatarini kunyimwa misaada ya kifedha kwa kukosa kujibu barua kuhusu haki
SERIKALI ya Kenya inakabiliwa na vikwazo, mmoja yao ikiwa ni kupunguziwa misaada ya kifedha kutokana na kuendelea kukiuka haki za kibinadamu nyakati za maandamano.
Shirika la Kutetea Haki za Kibinadamu la Umoja wa Kitaifa (UNHRDs) limesema serikali imekuwa ikisusia vikao vyake vya kusaili dhuluma dhidi ya waandamanaji nchini.
Mkuu wa UNHRDs Mary Lawlor alisema serikali ya Rais William Ruto imefeli kujibu barua zake mbili ambako alizua maswali kuhusu kutekwa nyara kwa waandamanaji, mateso na kutoweka kwa wakosoaji wa serikali kwa njia tatanishi.
Kupitia mtandao wake wa X, Bi Lawlor alifichua kuwa mnamo Oktoba 1, 2024 aliandikia Kenya barua kuhusu kamatakamata za kiholela, kuzuiliwa kwa waandamanaji, kuteswa kwao kisha kufurushwa kwa wapiganaji wa haki za kibinadamu.
Kwenye barua hiyo pia alitaka ufafanuzi kuhusu matumizi ya nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanaji waliovamia Bunge mnamo Juni 25.
Vijana hao wa Gen Z walikuwa wakipinga Mswada wa Fedha 2024 ambao ulikuwa umependekeza nyongeza ya ushuru.
Barua hiyo ililenga kufahamisha utawala wa sasa kuwa UNHRDs ilikuwa imepokea malalamishi ya ukiukaji wa haki za kibinadamu, vyombo vya habari na wanaharakati.
Mnamo Agosti 5, 2025, UNHRDs tena iliandikia serikali barua kuhusu kuandamwa kwa waandamanaji waliojibwaga barabarani mnamo Juni, 2025.
“Licha ya kuandikia serikali barua kuhusu masuala haya. Nasikitika kwamba sikupata jibu,” Bi Lawlor akaandika kwenye X huku akisema kuwa hadi leo kuna wanaharakati na waandamanaji waliotoweka na hawajawahi kupatikana.
Serikali ilihitajika kujibu barua hizo mbili ndani ya siku 20.
Aliyekuwa Mwanasheria Mkuu Justin Muturi alisema hakufahamu chochote kuhusu barua hizo.
“Niliondoka afisi ya mwanasheria mkuu mnamo Julai 11, 2024,” akasema Bw Muturi.
Juhudi za kupata kauli za Mwanasheria Mkuu Dorcas Oduor na Katibu katika Wizara ya Masuala ya Kigeni Korir Singóei hazikuzaa matunda kwa sababu hawakujibu jumbe kwenye simu zao.
Serikali kukosa kujibu barua hizo sasa kunafikisha suala hilo mbele ya Baraza la Umoja wa Kitaifa kuhusu Haki za Kibinadamu (UNHCR) ambalo lina mamlaka ya kuwekea serikali vikwazo ikiwemo kuwazuia wanachama wake kuipa Kenya msaada wa kifedha.