Kenya ilikopa Sh776.6M kila siku ndani ya miezi minne deni la nchi likigonga Sh12T – Ripoti
LICHA ya ahadi ya Rais William Ruto kuwa angepunguza deni la nchi, Kenya inazidi kukopa, Waziri wa Fedha John Mbadi akifichua kuwa deni la nchi sasa limefikia Sh12 trilioni.
Ndani ya miezi minne iliyopita, takwimu za Hazina Kuu ya Fedha zinaonyesha kuwa Kenya ilikopa Sh32.4 milioni ndani ya saa moja.
Stakabadhi zilizowasilishwa na hazina hiyo kwa Bunge la Kitaifa mnamo Oktoba 7, zilionyesha kuwa Kenya ilikopa Sh95.5 bilioni kati ya Mei 1, 2025 hadi Agosti 31, 2025 kugharimia miradi mbalimbali ya maendeleo.
Ukipiga hesabu, takwimu hizo zinaonyesha Kenya ilikopa Sh23.9 bilioni kila mwezi, Sh776.6 milioni kila siku, Sh539,321 kwa dakika na Sh8,988 kwa sekunde ndani ya miezi minne.
Mikopo hiyo ilitolewa kwa sarafu ya dola za Amerika na pia Euro.
Sheria zinazosimamia fedha za umma zinamhitaji Waziri wa Fedha ambaye anasimamia Hazina Kuu ya Kifedha aeleze bunge kuhusu kiwango cha deni la nchi.