Kenya yafanikiwa kutokomeza ugonjwa wa malale baada ya miaka 104
BAADA ya miaka 104 ya juhudi zisizokoma na wahudumu wa afya waliojitolea kwa dhati bila kukata tamaa, hatimaye Kenya imefanikiwa kuangamiza ugonjwa wa malale nchini.
Ijumaa iliyopita Shirika la Afya Duniani (WHO) lilitangaza rasmi kuwa Kenya haina tena visa vya ugonjwa huo unaojulikana kisayansi kama Human African Trypanosomiasis (HAT).
Mtu wa mwisho kuugua HAT nchini alipatikana mwaka 2009. Taifa limefanikiwa kupiga hatua kubwa katika safari hiyo iliyoanza mwaka 1901.“Napongeza serikali na wananchi wa Kenya kwa mafanikio haya ya kihistoria,” alisema Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt Tedros Adhanom Ghebreyesus.
“Kenya sasa imejiunga na orodha ya mataifa yaliyo huru bila ugonjwa huu. Hii ni hatua nyingine nzuri katika juhudi za kuwepo kwa bara Afrika lisilo na magonjwa yaliyopuuzwa,” alieleza.
Ugonjwa wa malale husababishwa na vimelea vinavyoitwa Trypanosoma. Nchini Kenya chanzo kikuu kilikuwa mbu.“Tangu 2009 hatujapata tena kisa chochote nchini.
Ufanisi huu ulitokana na hatua tuliyochukua ya kutekeleza mbinu jumuishi za wadau na sekta mbalimbali,” alieleza Dkt Seth Onyango, Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Kitaifa la Kuangamiza Mbung’o na Ugonjwa wa Trypanosomiasis (Kenttec), wakati wa hafla ya kusherehekea mafanikio hayo jijini Nairobi.
Timu ya Kenttec inajumuisha wataalamu kama Dkt Pamela Olet, Dkt. Monicah Maichomo (KALRO), Dkt Dunstan Mukoko, Dkt Joyce Onsongo (WHO), Prof Joseph Ndungu (FIND), Wyckliff Omondi (Mkuu wa Magonjwa Yaliyopuuzwa katika Wizara ya Afya), Dickson Kioko (Katibu wa NTDs), na Shirika la Huduma za Wanyamapori Nchini (KWS).
“Mafanikio haya yametokana na uongozi wa Wizara ya Afya, kujitolea kwa wahudumu wa afya katika maeneo yaliyo hatarini, na usaidizi kutoka kwa wadau muhimu,” alisema Dkt Abdourahmane Diallo, Mwakilishi wa WHO nchini.Ufanisi huu unakujia takriban miaka minane baada ya Kenya kuangamiza pia ugonjwa wa mnyoo wa Guinea.
“Hii ni dalili kuwa inawezekana kuondoa kabisa magonjwa yote yaliyopuuzwa nchini kupitia ushirikiano wa dhati,” alisema Dkt Meshack Ndirangu, Mkurugenzi wa Amref Health Africa nchini Kenya.
Mkurugenzi Mkuu wa Afya, Dk Patrick Amoth, alisema hatua hii inaonyesha jitihada za Kenya kwa miaka mingi, kupitia ushirikiano kati ya serikali za kitaifa na kaunti, taasisi za utafiti, washirika wa maendeleo na jamii zilizoathirika.
Amref inashirikiana na Wizara ya Afya kuangamiza magonjwa kama matende Kala-azar, kichocho na minyoo ya utumbo baadhi yakilengwa kutokomezwa ifikapo 2027 kulingana na Mpango wa Kitaifa wa Kenya wa mwaka huo.
“Hadi sasa, tumetoa zaidi ya dozi milioni 25 za matibabu dhidi ya kichocho, minyoo ya utumbo, na matende,” alisema Dkt Ndirangu.