Habari za Kitaifa

Kenya yawekwa ‘orodha ya aibu’ ya mataifa yenye ukatili kwa raia

Na ERIC MATARA July 31st, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KENYA sasa imo miongoni mwa mataifa sita mapya yaliyoongezwa kwenye orodha ya nchi zilizo na hali inayozorota ya uhuru wa raia.

Nchi nyingine zilizojiunga na orodha hiyo ni El Salvador, Indonesia, Uturuki, Serbia, na Amerika.

Hatua hii imejiri wiki chache baada ya maandamano ya Juni 25 na Julai 7, ambapo watu zaidi ya 60 waliuawa na mamia kujeruhiwa.

CIVICUS Monitor, shirika la kimataifa linalofuatilia hali ya haki za binadamu na uhuru wa kiraia katika mataifa 198, limeiweka Kenya kwenye orodha ya mataifa yenye hali ya kutia wasiwasi, likitaja “kuongezeka kwa kasi kwa ukandamizaji unaoendeshwa na serikali dhidi ya uhuru wa raia.”

Katika taarifa yake Jumatano, CIVICUS Monitor ilisema kuwa zaidi ya mwaka mmoja tangu maandamano ya #RejectFinanceBill ya Juni 25, 2024, serikali ya Kenya imeendelea kutumia mbinu za kikatili kunyamazisha sauti pinzani, zikiwemo matumizi ya nguvu hatari, kukamatwa kiholela na ujasusi wa kidijitali.

“CIVICUS Monitor imebadilisha orodha yake, na Kenya sasa iko miongoni mwa mataifa 51 duniani yanayoshuhudia kuporomoka kwa uhuru wa kiraia na haki za binadamu. Kenya imeorodheshwa katika kiwango cha pili kibaya zaidi kinachoweza kutolewa kwa nchi, kuonyesha kuwepo kwa vikwazo vikubwa dhidi ya uhuru wa kujieleza, kuandamana kwa amani, na kushirikiana,” alisema Ine Van Severen, Mkuu wa Utafiti wa raia wa CIVICUS.

“Jinsi serikali inavyokabiliana na maandamano ya amani imevuka kiwango hatari. Ukandamizaji huu wa mfumo unaonyesha mkakati wa makusudi wa kuharamisha ushiriki wa raia na kunyamazisha upinzani,” aliongeza.

CIVICUS ni muungano wa kimataifa wa mashirika ya kiraia na wanaharakati wenye wanachama zaidi ya 15,000 kutoka nchi 175. Washirika wake ni pamoja na Amnesty International, Oxfam, Greenpeace, Plan International na Save the Children.

Shirika hilo linatumia data kutoka kwa zaidi ya mashirika 20 ya utafiti na kutumia mfumo wa upangaji wa viwango kutoka “wazi” hadi “kufungwa kabisa”.

Kwa sasa, Kenya imeorodheshwa kama nchi “iliyofungwa,” kiwango kibaya zaidi.

Bw Van Severen alieleza kuwa mataifa yaliyo katika kiwango hicho huwa yamebanwa mno, na watu au mashirika yanayokosoa serikali huandamwa kwa kupelelezwa, vitisho, unyanyasaji, kifungo, majeraha au hata kuuawa.

Kulingana na shirika hilo, mnamo Juni 25, 2025, maelfu ya Wakenya waliingia barabarani kuadhimisha mwaka mmoja tangu maandamano ya 2024 ya #RejectFinanceBill, wakitaka mageuzi ya kiuchumi na ya kiutawala. Hata hivyo, serikali ilijibu kwa kutumia nguvu kali badala ya kusikiliza malalamishi yao.

Matukio hayo yameandikwa katika ripoti mpya ya CIVICUS iitwayo “Risasi za Polisi, Minyororo ya Kidijitali: Unyama wa Serikali Dhidi ya Uasi wa Amani unaoongozwa na Vijana Nchini Kenya.”

“Waandamanaji wasiopungua 65 waliuawa, mamia kujeruhiwa, na zaidi ya watu 1,500 kukamatwa. Ziliripotiwa visa vya ubakaji na ubakaji wa makundi, vinavyodaiwa kufanywa na wahuni waliotumwa na serikali kuingia kwenye maandamano, kuwashambulia waandamanaji na kupora biashara,” taarifa ilisema.