KEPHIS yapendekeza adhabu kali kwa wauzaji wa mbegu bandia
TAASISI ya Mbegu na Ustawishaji wa Mimea Nchini (KEPHIS) inashinikiza kuwepo kwa adhabu kali dhidi ya wafanyabiashara wanaoshiriki uuzaji wa mbegu feki na ambazo hazijathibitishwa.
KEPHIS, shirika la kiserikali linalosimamia ubora wa pembejeo na mazao ya kilimo, hasa afya ya mimea, ina jukumu kuhakikisha kuwa mbegu na mimea, zinaafiki viwango vya kitaifa na kimataifa vya ubora, afya, na usalama.
Hata hivyo, taasisi hii inahofia kwamba washirika wa utengenezaji na uuzaji wa mbegu feki mara nyingi huachiliwa kwa faini ndogo wanapofikishwa mahakamani.
“Tunashinikiza kuwepo kwa adhabu kali kwa sababu wahalifu hawa wanatengeneza mamilioni ya pesa kutokana na biashara hii haramu ya mbegu bandia,” anasema Bw Simon Maina, Mkurugenzi wa Uthibitishaji wa Mbegu na Aina ya Mimea KEPHIS.

Takwimu za taasisi hiyo zinaonyesha kuwa hadi kufikia mwaka uliopita, 2024, zaidi ya kesi 15 za ulaghai wa mbegu ziliripotiwa.
Kwa sasa, washirika katika biashara hii hatari kwa sekta ya kilimo – wanaopatikana na hatia, huadhibiwa faini ya Sh1 milioni au kifungo cha hadi miaka miwili jela.
Kulingana na KEPHIS, adhabu hiyo ni mithili ya tone la maji baharini au ziwani ikizingatiwa kuwa wahuni hao huunda mamilioni ya pesa.
Bw Maina anaelezea masikitiko yake, akisema baadhi ya wahusika huachiliwa kwa faini ndogo, hali inayofisha juhudi za kupambana na tatizo hili sugu.

“Kuahirishwa kwa kesi, mchakato mrefu wa mahakama, faini za chini, na ukosefu wa mamlaka kushtaki ni baadhi ya changamoto tunazokumbana nazo,” aelezea.
Taasisi hiyo inategenea Idara ya Polisi (NPS) na ya Uhalifu wa Jinai (DCI), pamoja na Afisi ya Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka ya Umma (DPP) kukabiliana na matapeli.
Kwa kuwa wakulima, hasa wale wa mashamba madogo, tayari wanapambana na athari za mabadiliko ya tabianchi, KEPHIS inasisitiza haja ya kuchukua hatua madhubuti ili kuimarisha mfumo wa mbegu, ikiwemo kuongezwa kwa adhabu kali dhidi ya wahalifu wa biashara hii haramu.
