Habari za Kitaifa

Kesi ya Sonko kuhusu wizi wa Sh357 milioni nayo yaanguka

February 7th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA RICHARD MUNGUTI

MAHAKAMA ya kukabiliana na kesi za ufisadi imemwachilia Gavana wa zamani wa Kaunti ya Nairobi Mike Mbuvi Sonko dhidi ya mashtaka ya wizi wa Sh357 milioni.

Bw Sonko alikuwa anakabiliwa na mashtaka hayo tangu 2019 ila katika miezi ya hivi punde kesi hiyo ilianza kuyumba kutokana na baadhi ya mashahidi kukosa kufika mahakamani.

Mnamo Novemba, mahakama hiyo ilimtaka Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Renson Ingonga kuwasilisha ushahidi katika kesi hiyo ya ufujaji wa Sh357 milioni dhidi ya Bw Sonko na washtakiwa wengine 16.

Hakimu mkuu Bi Eunice Nyuttu alimpa Bw Ingonga fursa ya mwisho kuwasilisha ushahidi katika kesi hiyo ambayo iliwasilishwa kortini miaka minne iliyopita.

Bi Nyuttu alikataa kutupilia mbali kesi hiyo na kumpa fursa ya mwisho DPP awasilishe ushahidi dhidi ya washtakiwa hao wote 17 waliomweleza “hawana hatia.”

Bi Nyuttu aliombwa atupe kesi hiyo kwa vile kiongozi wa mashtaka Bi Annette Wangia hajafika kortini mara tatu.

Ijapokuwa Bi Wangia alisemekana ni mgonjwa, hakimu alisema “hakuna afisa yeyote kutoka afisi ya DPP amejitokeza kueleza kuhusu ugonjwa wa Bi Wangia ama kuwasilisha stakabadhi za hospitali zikieleza kuhusu hatma yake.”

Bi Nyuttu alisikitika kesi hiyo imeahirishwa mara tatu mwezi huu na hakuna sababu maalum imewasilishwa na DPP.

Lakini Jumatano, mahakama hiyo ilitupilia mbali kesi hiyo ikisema hakukuwa na ushahidi wa kutosha kuiendeleza.

Soma: Kesi ya Sonko hatarini kuenda na maji DPP akipewa nafasi ya mwisho kuwasilisha ushahidi