Kesi ya ufisadi wa Sh357 milioni ya Sonko yafufuka
ALIYEKUWA Gavana wa Nairobi Mike Sonko amepata pigo baada ya Mahakama Kuu kubatilisha kuachiliwa kwake katika kesi ya ufisadi iliyohusisha Sh25 milioni, karibu miaka miwili iliyopita.
Jaji Nixon Sifuna Jumatano alifutilia mbali kuachiliwa kwa Bw Sonko, akisema hakimu aliyesikiliza kesi alifanya makosa katika uamuzi aliotoa Desemba 21, 2022 kwa kutegemea karatasi ya mashtaka ambayo ilirekebishwa na Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DDP).
Hakimu wa mahakama hiyo Douglas Ogoti alimwachilia Bw Sonko pamoja na ROG Security Ltd na Anthony Otieno Ombok, almaarufu Jamal, akisema, karatasi ya mashtaka iliyowasilishwa na upande wa mashtaka ilikuwa na dosari.
“Kwa hiyo, hakimu alifanya makosa makubwa alipotegemea karatasi ya mashtaka ambayo ilifanyiwa marekebisho kufikia uamuzi wake. Hii ni sawa na kutumia mfumo mbaya wa kusahihisha mtihani. Kwa hili pekee, uamuzi uliotajwa haufai,” alisema Jaji.
Jaji aliagiza Bw Sonko na Bw Ombok wafike mbele ya mahakama ya kusikiliza kesi za ufisadi ya Milimani mnamo Jumatatu, Desemba 16 ili kupata mwelekeo zaidi.Alisema hakimu mpya anafaa kutoa uamuzi ndani ya siku 30 iwapo Bw Sonko na Bw Ombok wana kesi ya kujibu au la, kulingana na ushahidi uliopo.
Bw Sonko, kupitia kwa wakili Dkt John Khaminwa, alisema atakata rufaa dhidi ya uamuzi huo baada ya ombi lake la kutaka kusitishwa kwa uamuzi kukataliwa na jaji. Jaji aliagiza kesi hiyo iwasilishwe mbele ya mahakama ya kupambana na ufisadi Jumatatu itoe mwelekeo.
Bw Sonko alikuwa ameshtakiwa kwa makosa manane, likiwemo la kula njama ya kushiriki ufisadi, mgongano wa kimaslahi, ulanguzi wa fedha, na kupata mapato ya uhalifu.
IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA