• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
Kevin Kang’ethe afuta mawakili, apunguza mbio za kumsafirisha Marekani

Kevin Kang’ethe afuta mawakili, apunguza mbio za kumsafirisha Marekani

NA RICHARD MUNGUTI

MKURUGENZI wa Mashtaka ya Umma (DPP) Renson Ingonga ameeleza mahakama ya Milimani, Nairobi kwamba amekamilisha kuandaa ushahidi utakaotegemewa katika kesi ya mauaji inayomkabili Mhadisi wa Ndege nchini Marekani, Bw Kevin Kang’ethe.

Bw Ingonga alimweleza hakimu mkuu wa mahakama ya Milimani Lucas Onyina kwamba amemkabidhi Kang’ethe nakala za ushahidi utakaotegemewa nchini Marekani aanze kujiandaa.

Bw Onyina alielezwa kuwa chini ya sheria za kimataifa, lazima ushahidi wote uwasilishwe mbele ya mahakama ya Kenya kabla ya mshukiwa kusafirishwa hadi ng’ambo kujibu mashtaka.

DPP alifahamisha Bw Onyina kwamba yuko tayari kuuwasilisha ushahidi dhidi ya Bw Kang’ethe ili mahakama itoe uamuzi ikiwa yuko na kesi ya kujibu au la.

Kiongozi wa mashtaka Bw Vincent Monda alieleza hakimu kwamba ushahidi umekabidhiwa mshtakiwa aandae tetezai zake.

“Mshukiwa huyu wa mauaji amekabidhiwa nakala za ushahidi wote aanze kuandaa tetezi zake atakazowasilisha kortini kupinga asirudishwe Amerika kushtakiwa,” Bw Monda alimweleza hakimu.

Bw Monda alisema kukabidhiwa kwa nakala hizo za mashahidi ni ishara DPP amejitolea.

Hakimu aliombwa aamuru kesi hiyo itajwe Machi 1, 2024, kwa maagizo zaidi.

Bw Monda alisema afisi ya DPP imejikakamua kukamilisha kesi hiyo humu nchini kwa haraka ili Bw Kang’ethe asafirishwe hadi Mahamkama Kuu mjini Boston jimbo la Massacheussetts, Marekani kufunguliwa shtaka la kumuua aliyekuwa mpenziwe, marehemu Margaret Mbitu.

Margaret alikuwa na umri wa miaka 30 alipouawa kwa kukatwa koo na kudungwa kwa kisu mara kadhaa.

Baada ya kuuawa, inadaiwa Bw Kang’ethe alimweka ndani ya gari aliloliacha katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Boston alipokuwa akifanya kazi na kutorokea nchini Kenya.

Bw Kang’ethe aliomba apewe muda kutafuta wakili wa kumtetea akisema “mawakili Antony Kago na David Muthama wamekoma kunitetea katika kesi hii”.

Bw Kevin Kang’ethe akiwa kizimbani Februari 27, 2024. Anatakiwa nchini Marekani kufuatia mauaji ya Margaret Mbitu. PICHA | RICHARD MUNGUTI

Alieleza mahakama katika kipindi cha mwezi mmoja, ameteseka sana lakini “Mabw Kago na Muthama walinyamaza kimya huku polisi wakiendelea kunitesa.”

Kang’ethe alisema ni haki yake kumsaka wakili atakayemwakilisha katika kesi hiyo kupinga asipelekwe nchini Marekani.

Bw Onyina alikubali ombi la Bw Kang’ethe kumsaka wakili wa kumtetea.

Hakimu aliorodhesha kesi hiyo itajwe tena Machi 1, 2024, ambapo Bw Kang’ethe ataeleza ikiwa atakuwa amempata wakili wa kumtetea.

Mshukiwa huyo inadaiwa alimuua Margaret baina ya Oktoba 30, 2023, na Novemba 4, 2023, na kufungia maiti yake ndani ya gari lake na kuliegesha katika garaji katika uwanja wa Boston.

Baada ya kesi hiyo kutajw, familia ya marehemu kupitia wakili Ngaruiya Gitau na Bi Margaret Njoroge, ilielezea masikitiko yao kwamba kesi hiyo imechukua muda kabla ya Bw Kang’ethe kurudishwa nchini Marekani.

“Watu wa familia ya marehemu wanasubiri haki itendeke kwa vile Margaret hakustahili kufa kinyama jinsi ile,” alisema Bi Njoroge ambaye ni shangazi ya marehemu.

Bi Njoroge mwenye umri wa miaka 70 alisema: “Niliona maiti ya Maggie. Alikuwa amechinjwa kama mnyama. Maiti yake iliraruliwa jinsi ambavyo mnyama wa mwituni hurarua windo lake. Tunataka haki ifanyike na sheria imwadhibu Bw Kang’ethe.”

Bw Onyina aliamuru kesi hiyo itajwe Machi 1, 2024, kwa maagizo zaidi.

  • Tags

You can share this post!

Zari asema hajaingiza mdudu kwa penzi la Mondi na Zuchu

Pokot Magharibi yamwaga kitita cha Sh600m kupiga jeki elimu

T L