KFCB yatembeza bakora kwa wasanii wa muziki ‘mchafu’
NA WANDERI KAMAU
JE, Bodi ya Kudhibiti Filamu Kenya (KFCB) itafanikiwa kuwakomesha wanamuziki wanaotunga nyimbo za kuipotosha jamii?
Hilo ndilo swali liloibuka Jumatano, baada ya bodi hiyo kutoa onyo kali kwa wanamuziki Chris Embarambamba na William Getumbe, kwamba itatoa nyimbo zao kwenye mtandao wa YouTube kwa kukiuka maadili ya kijamii na kidini.
Kwenye taarifa, Kaimu Afisa Mkuu Mtendaji wa bodi hiyo, Bw Christopher Wambua, alisema wamewaandikia barua wanamuziki hao wawili na kuwaagiza watoe nyimbo hizo kutoka mitandao yote ya kidijitali.
Baadhi ya nyimbo ambazo bodi hiyo ilirejelea ni ‘Niko Uchi’ wake Embarambamba na ‘Yesu Ninyan***’, wake Getumbe.
Bodi pia ilisema imeiagiza mitandao hiyo kuondoa nyimbo hizo, ikiwa wasanii hao hawataziondoa.
Hata hivyo, wadadisi wa masuala ya burudani wanasema kuwa huenda agizo hilo likakosa kupata mashiko, ikiwa bodi haitaweka mikakati kuhakikisha kuwa msanii yeyote anayetoa nyimbo za kupotosha jamii au zinazokiuka masuala ya kidini amekabiliwa vikali.
Wanasema kuwa hiyo si mara ya kwanza kwa baadhi ya wasanii—hasa Embarambamba—kutoa nyimbo zinazokiuka kanuni za kidini, na onyo kutolewa dhidi yake, ijapokuwa ameendelea kutoa nyimbo zinazokiuka kanuni za kijamii, kimaadili na hata kidini.
“Hii si mara ya kwanza tunaona bodi ikitoa onyo kwa wasanii wanaotoa nyimbo zinazokiuka maadili ya kijamii. Huu umekuwa kama mtindo, kwani hakuna hatua madhubuti zinazochukuliwa dhidi ya wasanii wanaotoa nyimbo kama hizo,” asema Bw John Muchiri, ambaye ni mwanahabari mkongwe wa masuala ya burudani.
Baadhi ya nyimbo ambazo zishawahi kutolewa kutoka mitandaoni kwa kuonekana kueneza jumbe zisizofaa ni ‘Tarimbo’ na ‘Figa’ za kundi la Ethic, ‘Vitamin U’ wao wanamuziki Timmy T Dat na Rosa Ree (kutoka Tanzania), ‘Taka Taka’ wake Alvindo kati ya nyingine.
Nyimbo nyingi zilitolewa baada ya maagizo yaliyotolewa na aliyekuwa Afisa Mkuu Mtendaji wa bodi hiyo, Dkt Ezekiel Mutua.
Ijapokuwa kwa sasa Dkt Mutua anaongoza Chama cha Kusimamia Muziki Kenya (MCSK), anasema wakati umefika kwa wanamuziki kuanza kutathmini athari za baadhi ya nyimbo ama tungo wanazotoa kwa jamii.
Anasema kuwa hata ikiwa serikali itaweka adhabu kali kwa wanamuziki wanaotoa nyimbo za kuipotosha jamii, ni wakati wasanii waanze kutathmini athari za vitendo vyao, kwani hata wao ni wazazi.
“La muhimu hapa ni wasanii wenyewe waanze kutathmini athari za nyimbo zao. Je, zinalingana na maadili ya kijamii? Ni maswali wanayofaa kujiuliza kabla ya kutoa nyimbo hizo,” asema.
Hata hivyo, baadhi ya wadadisi wanasema kuwa serikali inafaa kuzipa nguvu taasisi kama KFCB, kuwashtaki na kuwapiga faini kubwa wasanii wanaotoa nyimbo za kuipotosha jamii kimakusudi.
“Lazima tuige nchi kama Tanzania, ambayo imelipa nguvu Baraza la Sanaa la Tanzania (BASATA) kuwaadhibu wanamuziki wanaokiuka kanuni za kisanaa zilizowekwa,” asema Bi Sheila Mwikali, ambaye ni mdadisi wa masuala ya burudani.