• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
Khalwale amtaka Toto afute ‘uongo’ mitandaoni na kumlipa fidia ya Sh200m

Khalwale amtaka Toto afute ‘uongo’ mitandaoni na kumlipa fidia ya Sh200m

NA RICHARD MUNGUTI

SENETA wa Kakamega Boni Khalwale amemtaka mfanyabiashara Cleophas Shimanyula almaarufu Toto kufuta matamshi na kauli zote alizorekodi akimhusisha na kifo cha mfanyakazi wake aliyeuawa na fahali.

Pia anamtaka Bw Toto amlipe fidia ya Sh200 milioni kwa kumharibia jina yeye na wake zake watatu.

Mbali na kufuta habari hizo za kumkejeli katika mitandao ya kijamii, Dkt Khalwale amemtaka Bw Toto amuombe msamaha na kuwaomba msamaha wake zake watatu aliowadunisha katika habari alizosambaza katika mitandao ya kijamii.

Kupitia kwa wakili Danstan Omari Dkt Khalwale ameeleza kwa masikitiko jinsi mfanyakazi wake Kizito Moi Amukune alivyouawa na fahali aliyekuwa akimfundisha kupigana.

Dkt Khalwale hufuga mafahali anaowatumia kupigana wakati wa sherehe za kitamaduni.

Mfanyakazi huyo alishambuliwa na kufumwa na pembe na fahali huyo, Inasio, hadi akaaga dunia.

Katika barua aliyomwandikia Shimanyula mnamo Februari 7, 2024, Dkt Khalwale amemtaka afute katika mitandao ya kijamii habari za ‘kudanganya’ kuhusu seneta huyo.

Mwanasiasa huyo mtajika amekana alimuua Kizito na ripoti ya upasuaji imebaini alifumwa na pembe ya fahali mnamo Januari 28, 2024.

Wakili Omari alieleza kwa undani jinsi Dkt Khalwale alivyojulishwa kuhusu mkasa uliompata mfanyakazi wake.

Bw Omari alisema endapo Bw Toto hatamuomba msamaha, mteja wake hana budi ila kumshtaki na kuomba mahakama imfidie seneta huyo Sh500 milioni.

Fahali huyo aliuawa kwa mujibu wa mila za Jamii ya Abaluhya.

Dkt Khalwale alimfuma mkuki, kisha kichwa kikatwa na kupelekwa mahala ambapo hakutambua.

Watu wa jamii ya Dkt Khalwale na majirani walikatakata fahali kwa vipande na kugawana nyama yake.

  • Tags

You can share this post!

Ubomoaji waacha nyanya,90, binti anayeishi na ulemavu...

Naibu Inspekta Jenerali wa polisi asimulia korti jinsi...

T L