Kibagendi, Duale wararuana Bungeni hasira zikipanda kuhusu ufaafu wa SHA
UHASAMA kati ya Waziri wa Afya, Aden Duale, na Mbunge wa Kitutu Chache Kusini Anthony Kibagendi ulijitokeza waziwazi Jumanne, waliporushiana maneno makali wakilaumiana moja kwa moja Bungeni.
Kikao cha Kamati ya Afya ya Bunge la Taifa kilivurugika kwa zaidi ya nusu saa baada ya Waziri na Mbunge huyo kurushiana maneno mazito kuhusu uadilifu wao binafsi.
Kamati hiyo, inayoongozwa na James Nyikal (Seme), ilikuwa imeitisha kikao hicho na Wizara ya Afya, Baraza la Magavana (CoG) na wadau wengine kujadili mapendekezo ya ripoti ya Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA) kuhusu matumizi ya fedha tangu kuanzishwa kwake na changamoto katika vituo vya afya.
Hata hivyo, kikao ambacho kilitarajiwa kujadili kwa kina masuala yanayohusu wananchi kiligeuka kuwa kivumbi cha malumbano, hali iliyosababisha baadhi ya wanachama, akiwemo naibu mwenyekiti Patrick Ntwiga, kuondoka kwa hasira.
Waziri Duale, ambaye alikuwa amejiandaa kujibu maswali sita yaliyotumwa kwake Ijumaa kupitia barua kutoka kwa karani wa Bunge, alionekana kushangazwa alipokabidhiwa ripoti mpya ya ukaguzi wa Kamati kuhusu hospitali nchini kikao kikiendelea.
Kwa mujibu wa Dkt Nyikal, ziara ya Kamati hiyo katika vituo vya afya ilibaini changamoto nyingi zinazohusiana na sera za kitaifa ambazo haziwezi kushughulikiwa katika ngazi ya hospitali binafsi bila mikakati thabiti ya kisera.
Ripoti hiyo iliorodhesha changamoto zinazokabili SHA ikiwemo matatizo ya mfumo wa malipo, ukosefu wa uwazi katika malipo ya SHA, kiwango kikubwa cha malipo kukataliwa, ukosefu wa mfumo wa kukata rufaa kwa malipo yaliyokataliwa, mfumo wa SHA kushindwa kufanya kazi hadi mara nne kwa mwezi, na matatizo ya alama za vidole kwa wazee.
Waziri Duale alionyesha kutoridhishwa na namna alivyokabidhiwa ripoti hiyo bila taarifa za awali, akilalamikia ukosefu wa haki.
“Mlinitumia barua chini ya Ibara ya 153 ya Katiba. Nilijiandaa kujibu maswali sita niliyopokea Ijumaa. Hii ripoti nimepata dakika tano tu zilizopita – si haki kwa Wakenya nijibu kitu ambacho sijakisoma,” alisema Duale.
Aliomba siku saba kupitia ripoti hiyo kabla ya kutoa majibu kamili, ombi ambalo mwenyekiti alilikubali.
Aidha, alisisitiza kuwa kwa mujibu wa kanuni za Bunge na maamuzi ya Spika wa zamani Justin Muturi na wa sasa Moses Wetang’ula, haikuwa sahihi kupewa ripoti wakati kikao kinaendelea.
Taratibu rasmi
Baadhi ya wanachama, akiwemo naibu mwenyekiti, walimshauri waziri aache kufuata taratibu rasmi kupita kiasi na ajadiliane nao kwa manufaa ya wananchi.
“Wacha tuachane na masharti, tujadiliane kwa hoja. Ni nani ataokoa Wakenya kutoka kwa taasisi binafsi zinazotoa huduma za umma?” alihoji Ntwiga.
Duale alisisitiza kuwa yeye na timu yake watajibu masuala yanayohusu Wizara ya Afya na SHA pekee, akionya Kamati dhidi ya “kuingiza stakabadhi kisiri” na kusisitiza kuwa maswali yote lazima yatumwe mapema kulingana na kanuni za Bunge.
Mbunge wa Nandi, Cynthia Jepkosgei, alisema si jukumu la Waziri kuwa na wasiwasi kuhusu kanuni za Bunge kuliko wabunge wenyewe.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Afya ya Baraza la Magavana, Abduswamad Nassir, alikubaliana na Waziri kuhusu muda wa ripoti, akisema masuala hayo yanahitaji juhudi za pamoja kutatuliwa.
Hapo ndipo Mbunge Kibagendi alipochemka, akimtaka Waziri kuacha “kuwahubiria” wabunge kuhusu kanuni za Bunge, akimtaja kama “shahidi mkorofi”, jambo lililozua mabishano makali kati yake na Waziri kwa muda mrefu kikaoni.
Duale aliwakemea wabunge Kibagendi na Jepkosgei akiwalaumu kwa kujaribu kumtisha, huku akimtaka mwenyekiti wa Kamati kuwalinda maafisa wa umma dhidi ya udhalilishaji wanapofika mbele ya Kamati za Bunge.
Zaidi ya hayo, aliwashutumu baadhi ya wanachama wa Kamati ya Afya kwa kuwa na mgongano wa maslahi na ushiriki wa kutiliwa shaka katika masuala ya SHA.
“Tulikuja Bungeni kwa sababu mliituita, si kwa kuwa hatukuwa na kazi ya kufanya. Nimekuwa katika jengo hili kwa miaka 20, na nitafuata kiapo nilichokula.
“Baadhi ya wanachama wenu wanamiliki vituo vya afya – vingine nimevifunga. Wengine walitaka nivunje kanuni za SHA.
“Bodi ya SHA itawaajiri wataalamu bora zaidi. Wengine walikuja kuniona kuhusu vituo vinavyofanyiwa uchunguzi.
“Namheshimu Rais, lakini sitacheza michezo ya kisiasa. Huduma ya Afya kwa Wote (UHC) ilikuwa wazo la marehemu Rais Kibaki – na magenge hayakutaka ifanikiwe,” alisisitiza Duale.