• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 12:05 PM
Kibarua akiri kuiba njugu karanga

Kibarua akiri kuiba njugu karanga

NA RICHARD MUNGUTI

KIBARUA aliyeiba njugu karanga kilo 15, ameiambia mahakama alikuwa akitafuta pesa za nauli kusafiri hadi mashambani kumwona mama yake mgonjwa na kumpeleka hospitalini.

Bw Daniel Mukhwana aliomba mahakama ya Milimani imsamehe na imwachilie huru akampeleke mama yake kwa matibabu.

Bw Mukhwana aliungama mbele ya hakimu mkazi mahakama ya Milimani Nairobi Bw Ben Mark Ekhubi kwamba aliiba njugu karanga zenye thamani ya Sh6,000.

Alipoulizwa na Bw Ekhubi sababu ya kuiba njugu hizo, Bw Mukhwana alijieleza.

“Ni ukweli niliiba njugu karanga kutoka kwa duka la Bi Jane Wanjiru Mburu ninayemfanyia kazi ya kuzikaranga kwa karai nikitumia makaa,” Bw Mukhwana aliungama.

“Ni sababu gani iliyokufanya uibe njugu hizi?” Bw Ekhubi alimwuliza mshtakiwa.

Akajibu Bw Mukhwana: “Mheshimiwa, niliiba hizi njugu kuziuza nipate nauli kusafiri hadi mashambani kumwona mama yangu ambaye ni mgonjwa. Yapata mwezi mmoja tangu augue. Nilipokea simu kwamba mama yangu mzazi ni mgonjwa sana na sina pesa za kulipa nauli niende kumwona.”

Mshtakiwa huyo alisema hana pesa kutokana na hali ngumu ya kiuchumi iliyomfanya aishi maisha ya uchochole.

“Madaktari wamekuwa kwa mgomo na mama yangu ameumia bila kupata msaada wa kimatibabu. Nilikuwa nataka niuze hizi njugu karanga nipate nauli ya kusafiri hadi nyumbani kisha nimpeleke katika kliniki ya kibinafsi,” akajitetea.

Mshtakiwa huyo alieleza mahakama kwamba Mkenya wa kawaida anayeishi maisha ya kubahatisha anasukumwa na umaskini akielekezwa katika njia ya umauti.

“Mimi naishi maisha ya kubahatisha na sina kazi maalum na wala sina taaluma niliyosomea. Nafanya kazi ya kibarua ninachopata. Kwa sasa ninaandaa njugu karanga za Bi Mburu na kuzipakia ndani ya karatasi tayari kuuzia wateja,” akasema.

Hakimu alifahamishwa na mshtakiwa kwamba shida na ugonjwa wa mama yake mzazi ndivyo vilimlemea hadi akashawishika kuiba.

Aliomba mahakama msamaha na kuahidi kutorudia makosa hayo.

Kiongozi wa mashtaka Virginia Kariuki alieleza mahakama kwamba Mukhwana alivunja duka la Bi Mburu katika soko la Tsunami eneo la Ngara usiku wa Mei 6, 2024.

Bi Kariuki alisema njugu karanga alizokuwa ameiba baada ya kuvunja duka hilo zilipatikana.

Kiongozi huyo wa mashtaka alizitoa njugu hizo mahakamani kama ushahidi na kuomba mahakama imrudishie mlalamishi Bi Mburu akaziuze.

“Naomba mahakama imrudishie mlalamishi njugu hizi akaziuze kwa vile mshtakiwa amekiri shtaka na anasubiri adhabu,” Bi Kariuki alimrai hakimu.

Bw Mukhwana alikiri alivunja duka la Bi Mburu na kuiba kutoka mle kilo 15 za njugu karanga zenye thamani ya Sh6,000.

Kabla yakupitisha hukumu, Bw Ekhubi aliamuru idara ya urekebishaji tabia imhoji mshtakiwa na watu wa familia yake kubaini ikiwa mama yake ni mgonjwa jinsi ilivyodaiwa kortini.

“Utapelekwa gereza la Industrial Area hadi Mei 16, 2024 ndipo idara ya urekebishaji tabia iwasilishe ripoti yako. Nitaamua adhabu nitakayopitisha baada ya kupokea ushauri wa idara hii ya urekebishaji tabia,” Bw Ekhubi aliagiza.

  • Tags

You can share this post!

Azimio wakosoa mbinu za serikali kukabiliana na mafuriko

MAONI: EACC iwe tayari kupambana na wezi wa pesa za mafuriko

T L