Habari za Kitaifa

Kijana Gen Z aliyepigwa risasi akiwa amevalia sare za shule azikwa simanzi ikigubika kijiji Karatina

Na STEPHEN MUNYIRI December 26th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

KIJANA mwanafunzi wa sekondari ambaye alipigwa risasi na polisi mjini Karatina, Kaunti ya Nyeri akiwa amevalia sare za shule wakati wa maandamano ya Gen Z alizikwa mkesha wa Krismasi huku familia ikililia haki.

Kennedy Maina alikuwa na risasi iliyokwama kwenye nyonga na alikuwa akiugua nyumbani hadi Desemba 16 wakati alipokimbizwa hospitali ya Karatina Level 4 alipolemewa na maumivu, baadaye akaaga dunia.

Maina alikalia mtihani wake wa KCSE Novemba akiwa na maumivu mengi ila hakuishi kuona matokeo.

Alizikwa nyumbani kwa babu yake eneo la Rigati, Desemba 24 huku waombolezaji wakibubujikwa na machozi na simanzi kwa kifo hicho cha kijana mdogo waliyemuita shujaa Gen Z.

Familia, marafiki, viongozi na wanaharakati wa haki walikemea ukatili wa polisi na kutaka afisa aliyehusika kukamatwa na kufunguliwa mashtaka.

Waombolezaji wabeba jeneza la Kennedy Maina aliyekufa kwa jeraha la risasi alilopata wakati wa maandamano ya Gen Z. Picha|Stephen Munyiri

Bw David Maina, mjomba wa marehemu alisema mpwawe alitoka hospitalini Septemba ila alirudishwa mara kadhaa akilalamikia maumivu makali kwenye tumbo.

“Siku aliyokufa, alilalamikia maumivu kwenye nyonga na tukamkimbiza hospitalini. Kwa bahati mbaya hakupona. Tunataka serikali ihakikishe kijana wetu amepata haki. Alikuwa mpita njia bila hatia wakati alipopigwa risasi,” akasema akizuia machozi.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Mathaithi Purity Kinyua alimuomboleza Maina kama kijana mpole, mtiifu akalalamikia jinsi alipigwa risasi akiwa amevalia sare za shule.

“Inahuzunisha sana kwamba alifanya mtihani wa KCSE ila hakuishi hadi akapokea matokeo yake. Naomba polisi aliyempiga risasi asiwahi kupata amani. Inashangaza kwamba mkono mrefu wa serikali ambao unafaa kulinda raia wake umegeuka kuwa mkono mrefu wa mauaji. Ken hakuwa na silaha na hakuwa tishio kwa yeyote,” Bi Kinyua akasema.