Habari za Kitaifa

Kikosi cha kufukua mizimu ya 2022

March 12th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA BENSON MATHEKA

MUUNGANO wa Azimio La Umoja One Kenya umemteua aliyekuwa Mwanasheria Mkuu Amos Wako kuongoza timu ya watu watatu itakayouwakilisha katika ukaguzi wa uchaguzi mkuu wa 2022.

Wanachama wengine ni seneta mteule wa zamani Judith Pareno na mtaalamu wa masuala ya mtandao Julius Njiriani.

Uteuzi huo unajiri siku tatu tu baada ya Kamati ya Kitaifa ya Majadiliano (NADCO) kuwasilisha ripoti yake kwa Rais William Ruto na kinara wa upinzani Raila Odinga.

Majina hayo yaliwasilishwa kwa Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetangula Jumatatu, Machi 11, 2024 na Kiongozi wa Wachache Opiyo Wandayi.

“Kwa mujibu wa ripoti hiyo (ukurasa 73 aya ya 263a), ningetaka, kwa niaba ya Muungano wa Azimio la Umoja One Kenya kuteua wafuatao kuwa wanachama wa Jopo Kukagua Mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa 2022,” Bw Wandayi alisema katika barua yake kwa Bw Wetang’ula.

“Leo (Jumatatu) nimemwandikia Spika nikiwasilisha majina ya watu watatu ambao watakuwa wanachama wetu katika jopo,” Wandayi alisema.

Alimuomba Spika Wetang’ula kufanikisha kuundwa kwa jopo hilo haraka ili liweze kutekeleza majukumu yake.

Kenya Kwanza, muungano wa Rais William Ruto, bado haujatangaza hadharani majina ya walioteuliwa kushiriki shughuli hiyo ambayo ni mojawapo ya mapendekezo ya ripoti ya NADCO yaliyopitishwa na Bunge la Kitaifa na Seneti kabla ya kukabidhiwa Rais Ruto na Bw Odinga.

Ripoti ya NADCO ilipendekeza kuundwa kwa jopo la wataalamu waliobobea kuchunguza taratibu za uchaguzi wa urais wa 2022.

Hatua hii hailengi tu kutathmini chaguzi zilizopita lakini pia inaweka msingi wa kuanzisha utaratibu thabiti kutathmini michakato ya uchaguzi siku zijazo.

Jopo hilo linafaa kuundwa siku 21 baada ya kupitishwa kwa ripoti ya NADCO.

Bunge liliidhinisha ripoti ya NADCO Februari 2024. Ripoti hiyo iliwasilishwa Bungeni Desemba 7, 2023, na Kimani Ichung’wah, Kiongozi wa walio wengi na Mwenyekiti Mwenza wa NADCO pamoja na kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka.

Tayari miswada tisa imewasilishwa Bungeni ili kuwezesha utekelezaji wa ripoti hiyo.

Wiki iliyopita, Raila Odinga, kiongozi wa Muungano wa Azimio, alielezea wasiwasi wake kuhusu vitisho vilivyotolewa na baadhi ya washirika wa Rais Ruto ndani na nje ya Bunge vilivyolenga kuzuia utekelezaji wa ripoti hiyo.

Vile vile, Baraza Kuu la Azimio lilionya washirika wa Kenya Kwanza, ndani na nje ya Bunge, dhidi ya kuhujumu ripoti hiyo.

“Tunaonya wanaohusika kwamba majaribio yoyote ya kuhujumu utekelezaji wa ripoti hiyo yatakuwa na athari hasi,” Azimio ilisema kwenye taarifa.

Walilaumu baadhi ya viongozi wa Kenya Kwanza dhidi ya kuchelewesha, kuvuruga au hata kuua ripoti ya NADCO, ambayo ni hati iliyojadiliwa wakisema iliondoa nchi katika ghasia na kupata amani inayoshuhudiwa leo.

“Hakuna mtu anayepaswa kuchukulia kuwa hali ya sasa ilipatikana kwa urahisi,” walisema.