Kikwazo kipya kwa safari ya Raila AUC
NA AGGREY MUTAMBO
MABADILIKO mapya ya sheria za Umoja wa Afrika (AU) yanaweza kumfungia nje kiongozi wa upinzani Raila Odinga.
Kanuni hizo mpya zinapendekeza kwamba, watakaowania kiti cha mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC) mwaka 2025 wawe wanawake.
Bw Odinga ameidhinishwa rasmi na serikali ya Kenya kuwania kumrithi Moussa Faki Mahamat wa Chad.
Lakini pendekezo lililosambazwa kwa nchi wanachama mnamo Jumanne linasema wagombea wa kike pekee ndio wanaohitimu katika uchaguzi ujao, ingawa kiti hicho kwa mzunguko kitatwaliwa na raia kutoka ukanda wa Afrika Mashariki.
Pendekezo hilo limo katika rasimu ya ripoti iliyofanyiwa marekebisho kuhusu maandalizi ya Uchaguzi wa Uongozi wa Tume ya Muungano wa Afrika utakaofanyika Februari 2025.
Ripoti hiyo imeandaliwa na Wakili wa AU na Afisi ya Naibu Mwenyekiti wa Tume, kwa kushirikiana na Kamati ya wawakilishi wa kudumu na inapaswa kuwasilishwa kwa Baraza Kuu la Muungano wa Afrika kuidhinishwa kabla ya kupitishwa.
Inasema nyadhifa za Mwenyekiti na Naibu Wenyekiti lazima zizingatie kanuni ya usawa wa kijinsia, ikimaanisha kwamba, wanaoshikilia nyadhifa hizo mbili hawawezi kuwa wa jinsia moja wakati wowote, desturi iliyoanzishwa mnamo 2021.
Lakini pia inasema, kwa mara ya kwanza kwamba, mtu aliye madarakani anapaswa kubadilishwa na mtu wa jinsia tofauti katika chaguzi zinazofuata.
“Kwa hivyo, kwa mujibu wa kanuni iliyotajwa hapo juu, mwenyekiti katika uchaguzi ujao wa 2025 lazima awe mwanamke. Kwa hivyo, wagombea wa kike pekee ndio watazingatiwa kwa wadhifa wa mwenyekiti, na wagombea wanaume pekee ndio wanaofaa kwa wadhifa wa Naibu Mwenyekiti,” ripoti inapendekeza.
“Ili kuzingatia kanuni ya usawa wa kijinsia wa mzunguko, imeamuliwa kuwa Mwenyekiti ajaye wa Tume awe mwanamke, na Naibu Mwenyekiti anayefuata awe mwanamume,” inasema.
Kumekuwa na mwanamke mmoja tu mwenyekiti wa AUC katika historia ya Muungano wa Afrika, Nkosazana-Dlamini Zuma wa Afrika Kusini ambaye alihudumu kwa muhula mmoja kati ya 2012 na 2017.
Hadi 2021, hakukuwa na kizuizi cha kuwa naibu mwenyekiti ingawa utaratibu ulikuwa naibu kutotoka ukanda mmoja na Mwenyekiti.
Naibu wa Dkt Zuma alikuwa Erastus Mwencha wa Kenya na naibu wa Faki katika muhula wake wa kwanza (2017-2021) alikuwa Thomas Kwesi wa Ghana.
Kwa sasa, Naibu wake ni Monique Nsanzabaganwa wa Rwanda.
Uchaguzi ujao wa AUC unatarajiwa kufanyika Februari mwaka ujao na ripoti hii inatakiwa kubuni sheria zitakazofuatwa, kwa kuzingatia muundo wa mageuzi wa kitaasisi wa AU 2018 kama ilivyopendekezwa na Rais wa Rwanda Paul Kagame.