Kilichofanya Lagat kushindwa kufuta kesi inayotaka aondoke ofisini
Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi Eliud Lagat ameshindwa katika jaribio la kufutilia mbali kesi inayolenga kuondolewa kwake ofisini kuhusiana na kifo cha mwalimu Albert Ojwang’ kilichotokea miezi minne iliyopita akiwa kizuizini.
Bw Lagat pamoja na Mwanasheria Mkuu Dorcas Oduor walitaka kesi hiyo iondolewe wakidai Mahakama Kuu haina mamlaka ya kushughulikia masuala ya ajira na uhusiano wa kikazi.
Jaji Chacha Mwita katika uamuzi wake alisema kuwa Mahakama Kuu ina uwezo wa kusikiliza masuala ya kikatiba yaliyoibuliwa na mlalamishi, mwanaharakati wa haki Eliud Karanja Matindi.
Hoja kuu ni iwapo uamuzi wa Bw Lagat wa “kujiondoa” kazini kwa siku 18 ili kuruhusu uchunguzi wa mauaji unafaa kuhesabiwa kama kujiuzulu, ingawa yeye alidai alikuwa likizo ya kiutawala.
Mahakama ilisema kesi hiyo inalenga kubaini uhalali wa hatua za Bw Lagat na uteuzi wa msaidizi wake Patrick Tito kama kaimu Naibu mkuu wa polisi. Pia, kuna swali kuhusu jukumu la Tume ya Huduma ya Polisi (NPSC) na iwapo ilitenda kisheria.
Bw Matindi anadai “kujiondoa” kwa Lagat kulikuwa sawa na kujiuzulu kwa mujibu wa Kifungu cha 12 cha Sheria ya Huduma ya Polisi. Anasema kitendo hicho kilisababisha mgongano wa kikatiba kwani kulitokea hali ambapo kulikuwa na Naibu wakuu wawili wa polisi, mmoja halisi na mwingine kaimu.
Hata hivyo, Bw Lagat anapinga akisema hakuwahi kujiuzulu bali alienda likizo iliyokuwa imeidhinishwa na Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja, ili kuruhusu Mamlaka ya kiraia ya kusimamia utendaji wa polisi (IPOA) kufanya uchunguzi kufuatia presha ya umma.
Kesi hii imeibua mjadala mkubwa kuhusu uwajibikaji wa makamanda wa polisi, tafsiri ya kikatiba ya “kujiondoa,” hasa baada ya ripoti za vifo zaidi ya 20 katika vituo vya polisi katika kipindi cha miezi minne.
Mahakama itasikiza kesi hii mnamo Novemba 17 2025.