Habari za Kitaifa

Kilichofanya Mahakama ya Juu kutupa kesi ya kutaka uchaguzi ufanyike 2026

Na  JOSEPH WANGUI August 15th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

Mahakama ya Juu zaidi nchini imetupilia mbali kesi iliyotaka tafsiri ya Katiba kuhusu tarehe ya uchaguzi mkuu ujao, ikisema kuwa haina mamlaka ya kuamua suala hilo.

Jopo lote la majaji wa Mahakama ya Juu likiongozwa na Jaji Mkuu Martha Koome, liliamua kwamba halikuwa na uwezo wa kisheria kushughulikia masuala yaliyowasilishwa na walalamishi, ambao ni wakili Dkt Owiso Owiso, mtetezi wa haki za binadamu Khelef Khalifa, na wakili Ashioya Biko.

Watatu hao waliwasilisha ombi lao Aprili 2025, wakitaka Mahakama ya Juu iamue kuwa uchaguzi mkuu ujao unapaswa kufanyika mwezi Agosti 2026,  na si 2027 kama ilivyopangwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka(IEBC).

Walidai kuwa uchaguzi ukifanyika 2027 utakuwa kinyume cha Katiba kwani ni zaidi ya miaka mitano tangu uchaguzi wa 2022, hivyo kumaanisha kuongezea  Rais William Ruto muda wa kuhudumu kinyume cha sheria.

Mahakama ilisema kuwa mamlaka yake ya kipekee chini ya Kifungu cha 140 cha Katiba huweza kutumika tu katika kushughulikia ushauri kuhusu uhalali wa uchaguzi wa urais  na si kuhusu tarehe ya uchaguzi.  Mamlaka hayo ni ya kipekee na hayawezi kutumiwa kuamua mizozo ya kabla ya uchaguzi kama vile suala la tarehe ya uchaguzi wa urais,” walisema majaji.

Mahakama ilieleza kuwa tafsiri ya Katiba kuhusu masuala kama haya yanapaswa kuwasilishwa katika Mahakama Kuu, ambayo ndiyo yenye mamlaka ya awali ya kusikiliza kesi za aina hiyo.

Pia walikosoa namna kesi hiyo ilivyowasilishwa, wakisema ilikuwa kinyume cha utaratibu, kwani walalamishi waliwasilisha kesi na kwa wakati huo huo wakaomba idhini ya kuwasilisha kesi hiyo hiyo.

“Ni utaratibu usioeleweka kisheria; huwezi kuwasilisha kesi halafu uombe ruhusa ya kuiwasilisha tena. Ni dhahiri kuwa hakuna msingi wa kisheria unaoruhusu hilo,” waliongeza.