Kimbunga Hidaya chahepa Kenya huku kikisukuma wavuvi wa Zanzibar hadi Lamu
KALUME KAZUNGU NA WACHIRA MWANGI
MABAHARIA kumi kutoka Zanzibar waliokolewa baada ya boti lao kusukumwa na mawimbi baharini hadi eneo la Kipini nchini Kenya, mpakani mwa kaunti za Lamu na Tana River, wakati wa machafuko ya bahari yaliyosababishwa na Kimbunga Hidaya.
Mabaharia hao walikuwa wameondoka Pemba, Zanzibar kuelekea Tanga, Tanzania wakati injini yao ilipogongwa na kuharibiwa na mawimbi makubwa yanayoaminika kusababishwa na kimbunga hicho.
Waokoaji waliozungumza na Taifa Leo walisema juhudi za mabaharia hao kujaribu kudhibiti jahazi hazikufua dafu, hali iliyopelekea kusombwa na maji kutoka Zanzibar hadi Kipini nchini Kenya kabla ya kufanikiwa kupata msaada wa kutia nanga.
Mwenyekiti wa Kitengo cha Usimamizi wa Ufuo wa Malindi (BMU), Bw Yunus Aboud Sahe, ambaye aliongoza kikosi cha kuwaokoa mabaharia hao, alisema wote kumi wako salama.
Bw Sahe alisema walipokea simu za kuomba msaada kutoka kwa mabaharia hao baada ya kufika Mombasa lakini bahari ilikuwa imechafuka na haingewezekana kuwasaidia.
“Tuliwasiliana nao walipofika Mombasa. Tulijaribu kufanya mipango ili wasaidiwe huko lakini ilikuwa vigumu kwa boti hiyo kutia nanga kutokana na mawimbi makubwa na upepo mkali baharini.
“Kwa hivyo, walisukumwa na mawimbi, kupita Mombasa, Kilifi, Malindi na hatimaye kati ya Kipini na Ziwayu ambapo tulifanikiwa kuwafuatilia na kufanikiwa kutia nanga. Tuliwaokoa wote kumi. Wako salama Lamu,” akasema Bw Sahe.
Mkurugenzi wa usimamizi wa majanga Kaunti ya Lamu, Bw Shee Kupi, alithibitisha kuokolewa kwa wanamaji hao kumi wa Zanzibar.
Afisa wa KCGS ambaye hawezi kutajwa jina kwa kukosa mamlaka ya kuzungumzia suala hilo, alithibitisha kisa hicho na kusema taarifa rasmi itatolewa baadaye.
Mjini Mombasa, mashirika ya usalama yalikuwa macho katika fuo za umma ili kuwaepusha watu kujaribu kuenda kuogelea.
Uchunguzi wa Taifa Leo katika ufuo wa umma wa Jomo Kenyatta ulio maarufu kama Pirates na ufuo wa Nyali mchana ulipata hapakuwa na shughuli yoyote.
Waliosalia ufuoni ni polisi na maafisa wa ukaguzi wa kaunti pamoja na wahudumu wa Msalaba Mwekundu wa Kenya.
Kimbunga hicho ambacho kilitua nchini Tanzania siku ya Jumamosi kilisababisha upepo mkali na mawingu meusi katika maeneo ya pwani ya Kenya.
Ingawa idara ya utabiri wa hali ya anga iliondoa hofu kuwa kimbunga hicho kingetua Mombasa, ilieleza kuwa huenda Pwani ya Kenya ikakumbwa na athari zake kupitia upepo mkali na mawimbi makubwa. Idara hiyo ilisema kuwa athari hizi zinatarajiwa kudumu hadi Jumanne.