Kimbunga Hidaya: Gavana Nassir apiga marufuku uvuvi, kutangatanga ufuoni
NA WACHIRA MWANGI
SERIKALI ya Kaunti ya Mombasa imechukua hatua za haraka katika kukabiliana na athari zinazotarajiwa za Kimbunga Hidaya, ikisimamisha shughuli zote za ujenzi, matembezi katika fuo na uvuvi baharini hadi Jumatatu usiku.
Akitoa maelekezo ya kulinda wakazi wa Mombasa, Gavana Abdulswamad Nassir alisisitiza umuhimu wa hatua za haraka mbele ya kimbunga kinachokuja.
Alitaka maafisa wa Kaunti, wakishirikiana na Polisi wa Kitaifa, Jeshi la Wanamaji la Kenya, na Kikosi cha Coast Guard, kuhakikisha utekelezaji wa agizo la kutoingia katika Bahari Hindi kwa wakazi hadi kimbunga kipite.
“Hakuna ruhusa ya kuingia baharini, na timu zetu za usalama zitadhibiti maeneo haya kwa uangalifu,” akasema Gavana Nassir.
Aidha, aliwaomba mameneja wa hoteli kuchukua jukumu la kukataza wageni dhidi ya kutumia bahari hadi ukaguzi utakapofanyika usiku wa Jumatatu.
Gavana Nassir alisisitiza umuhimu wa hatua za tahadhari, ikiwa ni pamoja na kufunga visima na vidimbwi vya maji pamoja na kuimarisha miundo ya paa.
Aliamuru kufungwa kwa matimbo yote ili kupunguza hatari za ajali wakati kimbunga kinapopita.
“Maafisa wa Kaunti wamepewa jukumu la kuwaelimisha umma kuhusu hatua za usalama,” alisisitiza Gavana Nassir, akisisitiza umuhimu wa kipaumbele cha usalama wa binadamu kuliko mali.
Alisisitiza juhudi za pamoja za mashirika mbalimbali, ikiwa ni pamoja na Polisi wa Kitaifa, Jeshi la Wanamaji wa Kenya, na Huduma za Kikosi cha Coast Guard, katika maandalizi.
Akikiri udhaifu wa makazi yasiyostahili karibu na vijito, gavana Nassir alihakikisha hatua za kuwahamisha kwa utu.
Aliwahimiza wakazi kutumia nambari za dharura 0707911911 ikiwa msaada unahitajika, akisisitiza utayarifu na uimara wa wanajamii wote kukaa chonjo changamoto ikiwakodolea macho.
Kimbunga Hidaya kilifika nchini Tanzania na kinavyoelekea kwenye fuo za Mombasa na Pwabi ya Kenya kwa ujumla, kiongozi huyo alisisitiza umuhimu wa kuwa tayari, akielezea uwezekano wa kutokea athari za baada ya kimbunga chenyewe.
Aliwahimiza wakazi kuendelea kuwa macho na kushirikiana na mamlaka katika kulinda maisha na mali.