Kinachopeleka walimu 10,000 ikulu kukutana na Ruto
Maafisa wa serikali kuu pamoja na viongozi wa vyama vya walimu na mashirika yao walikutana Ijumaa katika maandalizi ya dakika za mwisho ya mkutano mkubwa na Rais William Ruto utakaofanyika Ikulu, Nairobi leo Jumamosi.
Mnamo Jumatano, viongozi hao walikutana na Katibu wa Wizara ya Elimu ya Msingi, Prof Julius Bitok, katika makao makuu ya wizara, Jogoo House, ambapo walikubaliana kuhusu wawakilishi wa walimu kwa hafla hiyo ambayo inatazamwa kama ya kihistoria.
Awali, mkutano huo ulikuwa umepangwa kufanyika Ijumaa na kuhudhuriwa na idadi ndogo ya wageni, lakini ukasongezwa hadi Jumamosi. Badala yake, Rais alialika ujumbe wa kisiasa kutoka Kaunti ya Murang’a siku hiyo, na siku ya Alhamisi alikuwa mwenyeji wa ujumbe kama huo kutoka Kisii.
Chama cha Kitaifa cha Walimu Kenya (KNUT) kimepewa nafasi nyingi zaidi – wawakilishi 3,300. Chama cha Walimu wa Sekondari (KUPPET) kitawakilishwa na walimu 2,000 huku Chama cha Walimu wa Elimu Maalum (KUSNET) kikipata nafasi 400 pekee.
Chama cha Wakuu wa Shule za Msingi (KEPSHA) kitawakilishwa na walimu 2,300, huku Chama cha Wakuu wa Shule za Sekondari (KESSHA) kikipokea nafasi 2,000.
Waziri wa Elimu Julius Ogamba alikutana na viongozi wa vyama hivyo kutoa mwelekeo kuhusu jinsi watakavyowasilisha hoja zao kwa Rais. Ilielezwa kuwa ni makatibu wakuu wa vyama na wenyeviti wa mashirika tu ndio watakaozungumza rasmi.
Mkutano wa saa mbili na Prof Bitok ulilenga kuweka ajenda ya mjadala na kukamilisha muundo wa ujumbe wa walimu 10,000 utakaokutana na Rais Ruto.
Miongoni mwa masuala yatakayojadiliwa ni hali ya maisha ya walimu, mazingira ya kazi, na nafasi ya walimu katika utekelezaji wa mageuzi ya elimu nchini.
Viongozi wa vyama hivyo walikubaliana kuwasilisha msimamo mmoja kuhusu masuala ya mshahara, marupurupu, na masilahi ya walimu, huku wakionyesha utayari wa kushirikiana na serikali katika mageuzi ya sekta ya elimu.
Msemaji wa Ikulu Hussein Mohammed alithibitisha kuwa mkutano huo unahusu masuala ya elimu pekee, akisema kuwa “Ikulu ni mahali pa umma na si mali ya watu fulani pekee”.
Mwenyekiti wa KEPSHA, Bw Fuad Ali, alisema kuwa mojawapo ya hoja kuu itakayowasilishwa ni ucheleweshaji wa fedha kwa shule – jambo ambalo limevuruga ratiba ya masomo na kulazimu baadhi ya wakuu wa shule kuwatuma wanafunzi nyumbani.
Vyama vya walimu pia vinatarajiwa kushinikiza utekelezaji wa mikataba ya pamoja ya kazi (CBAs), mazingira bora ya kazi, na ufafanuzi kuhusu msimamo wa serikali katika suala la michango ya pensheni.
Rais pia anatarajiwa kuwahakikishia wakuu wa shule kuhusu mfumo mpya wa ufadhili wa elimu ya juu, ambao umekumbwa na ukosoaji kwa kucheleweshwa kwa fedha na mkanganyiko miongoni mwa wazazi na wanafunzi.
Mkutano huu unakuja wakati ambapo shinikizo kwa serikali zimeongezeka kudhihirisha dhamira ya kutatua changamoto za elimu, huku mabadiliko ya mara kwa mara ya sera yakitishia uthabiti wa sekta ya elimu kwa walimu, wanafunzi, na wazazi.