Kinaya wanafunzi wakifukuzwa kuendea pesa za masomo ya ziada
NA WINNIE ATIENO
WAZAZI nchini wameingiwa na hofu baada ya walimu wakuu kuanza kufukuza wanafunzi shuleni kutokana na kutolipa karo na fedha za masomo ya ziada.
Hii ni licha ya serikali kupiga marufuku masomo ya ziada. Hata hivyo, walimu wakuu wamekuwa wakiendeleza masomo hayo na kulazimisha wazazi kugharamia.
Shule nyingi hutoza Sh1,000 kwa kwa mtoto kila muhula.
Walimu wakuu wamekuwa wakijitetea kuwa masomo ya ziada yanasaidia wanafunzi ambao hawafanyi vyema.
Hata hivyo, mwenyekiti wa kitaifa wa muungano wa wazazi nchini, Bw Silas Obuhatsa aliilaumu serikali kwa changamoto zinazokabili sekta ya elimu.
Alisema walimu wakuu hawana budi ila kufukuza wanafunzi kwenda kuchukua karo ya shule kutokana na kucheleweshwa kwa fedha za elimu kwa taasisi hizo.
Bw Obuhatsa alisema walimu wakuu wanapitia changamoto na gharama ya juu ya maisha kutokana na malimbikizi ya madeni, ukosefu wa karo za shule baada ya wazazi kudinda kulipa, na hata serikali kutosambaza fedha za elimu shuleni.
“Mnataka walimu wakuu waendeshe vipi sekta ya elimu bila fedha? Kwa upande mmoja, wazazi hawalipi karo na serikali inachelewesha fedha, hii ni hali ngumu jamani. Nilikutana na mwenyekiti wa kitaifa wa muungano wa shule za upili nchini, Bw Willy Kuria ambaye aliungama kuwa, hawajapokea fedha za muhula huu,” aliongeza.
Bw Obuhatsa alisema shule za upili zilipokea fedha muhula uliopita.
“Kulingana na Bw Kuria, serikali ilitoa asilimia 40 ya fedha shule zilipokuwa zikielekea kufungwa. Fedha nyingi zilitumika kulipa madeni. Alisema kila mwanafunzi alipokea Sh8,200 badala ya Sh11,122,” alisema Bw Obuhatsa.
Akiongea na Taifa Leo kwa njia ya simu, Bw Obuhatsa alisema serikali inafaa kutuma fedha za shule mapema ili kuwapa walimu wakuu wakati mwafaka kutimiza malengo yao.
Alisema walimu wakuu hawana budi ila kufukuza wanafunzi kuendea karo.
Vile vile, aliwasihi wazazi kulipa karo kwa wakati ufaao.
“Fedha za elimu zinafaa kutumwa kila muhula, wakati shule zinafunguliwa. Ama serikali ipeane mwongozo namna shule zinaweza kuendesha shughuli zao bila fedha,” aliongeza Bw Obuhatsa.
Alisema shule za mabweni zimeathirika zaidi na ukosefu wa fedha kwa sababu zinategemea karo.