Kindiki: Wakenya watosheke na ‘taifa moja, bendera moja’
NA MWANGI MUIRURI
NAIBU Rais Rigathi Gachagua anazidi kutengwa na mawaziri kutoka Mlima Kenya kuhusu mfumo wa ugavi wa rasilimali za taifa kwa kuzingatia idadi ya watu.
Baada ya Waziri wa Utumishi wa Umma Moses Kuria kusema mfumo huo unaoshabikiwa na Bw Gachagua haufai, sasa mwenzake wa Usalama wa Ndani Prof Kithure Kindiki amepinga.
Hii ni licha ya Bw Gachagua kutangaza hadharani kwamba wote wanaopinga mfumo huo kutoka Mlima Kenya ni wasaliti.
Hata hivyo, Bw Gachagua amepata jeki kuu katika kampeni yake baada ya kinara wa upinzani Bw Raila Odinga kutangaza kwamba anamuunga mkono.
Bw Gachagua alishawaagiza wenyeji kuwapiga msasa wote ambao ni viongozi wa kutoka Mlima Kenya “na yeyote ambaye atapinga mfumo wa ugavi wa rasilimali kwa kuzingatia idadi ya watu na kuhusu umoja wetu ahesabiwe kama msaliti”.
Tayari, mshauri mkuu wa Rais William Ruto kuhusu masuala ya kiuchumi Dkt David Ndii amesuta mfumo huo kama usiofaa.
Wengine ambao wamepinga ni pamoja na Mbunge wa Kangema Peter Kihungi na Seneta wa Nyandarua John Methu.
Akipinga kupitia akaunti yake katika mtandao wa X, Prof Kindiki alisema kwamba mfumo huo hauna upana wa kimawazo kuwafaa Wakenya wote na kuwataka wazalendo kuchangamkia mfumo wa Kenya moja, bendera moja.
Alisema kwamba wanaopigia debe mfumo huo wa idadi ya watu hawaelewi kuhusu madhara yake ya sasa na pia katika siku za usoni.
Alisema kwamba mfumo huo hauna mashiko ya kisheria, kiuchumi, na kisayansi “na hata hakuna takwimu za kuupa mjadala huo ufasaha wa kuuelezea”.