Kindiki anguruma, amchambua Gachagua kuliko awali
HATUA ya Naibu Rais Profesa Kithure Kindiki kumkaba koo mtangulizi wake Rigathi Gachagua, inaonekana kufungua uwanja mpya wa vita katika ubabe wa siasa za Mlima Kenya.
Profesa Kindiki, wikendi alimenyana na Bw Gachagua mitandaoni baada ya mtangulizi wake kudai alitumia Sh60 milioni kufadhili ghasia eneo la Mlima Kenya wakati wa maandamano.
Akiongea jijini Boston, Amerika Bw Gachagua alidai kuwa Rais William Ruto anamtumia Profesa Kindiki pia kumdhalilisha kisiasa Mlimani.
“Waliwalipa wahuni kuzua ghasia na uharibifu ili Wakenya watugeuke lakini watu si vipofu, waliona ukora huo,” akasema Bw Gachagua.
“Pesa ambazo anatumia kuzunguka na helikopta zingetumika kujenga na kukarabati hospitali na shule badala ya kutupwa tu kwa kisingizio cha kuinua watu kimapato. Vijana wanaona haya yote,” akaongeza Bw Gachagua.
Profesa Kindiki hata hivyo, alijitetea akisema kuwa kwa kipindi kirefu amekuwa siasani hajawahi kuhusishwa na ghasia zozote.
“Mtu wa mitego nimesikia ukisema nilifadhili wahuni, katika kipindi kirefu ambacho nimehudumu kama mtumishi wa umma, sijawahi kuhusishwa na uhuni,
“Ulijiporomosha mwenyewe kutokana na maringo yako mwenyewe na mtindo wako wa kuwavamia watu kutaharakisha tu upate adhabu yako,” akasema Profesa Kindiki.
“Hata kusema uongo huhitaji hekima kidogo. Unaandaa mchango na kuwakodisha mawakili kuwaokoa wahuni ambao walikodishwa na mtu mwengine?” akauliza.
Ubabe kati ya wanasiasa hao wawili unaonekana kuchangiwa na kila mmoja kuvutia kura za Mlima Kenya kuelekea kura ya 2027.
Rais alipozuru Kaunti ya Meru mnamo Juni 21 siku ambayo pia Bw Gachagua alikwepo, Profesa Kindiki alimwaambia Rais amwaachie jukumu la kupambana na upinzani eneo hilo.
“Leo ni rais amesimama hapa. Nataka nirudi nisimame hapa na kupambana na wanaume hao mwenyewe,” akasema Profesa Kindiki.
“Hawatujui, hawatuelewi na wanatupima wakifikiria sisi ni watu wadogo. Haya madharau na kiburi yataisha, ni muda tu,” akaongeza Profesa Kindiki.
Kwa mujibu wa mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Javas Bigambo, Profesa Kindiki anapambana kwa jino la ukucha kuhakikisha kuwa Rais Ruto anapata angalau zaidi ya kura milioni mbili kwenye kaunti za Meru, Tharaka-Nithi na Embu.
“Kindiki hana haja sana na kura za jamii ya Mlima Kenya Magharibi ambayo ni Agikuyu, analenga kura milioni mbili za Mlima Kenya Magharibi ili ajiweke pazuri kutetea wadhifa wake kama mgombeaji mwenza,” akasema Bw Bigambo.
Mchanganuzi huyo anasema kuwa hata kama Profesa Kindiki anazunguka maeneo mengine akishiriki michango ya kuyainua makundi mbalimbali, lengo lake ni kusalia na kura kaunti hizo tatu.