• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 7:47 PM
Kindiki aonya magenge ya ujambazi Magharibi mwa Kenya

Kindiki aonya magenge ya ujambazi Magharibi mwa Kenya

NA JESSE CHENGE

WAZIRI wa Wizara ya Usalama wa Ndani Kithure Kindiki ametoa onyo kali kwa magenge yanayotekeleza ujambazi Magharibi mwa Kenya.

Prof Kindiki alisema kuna genge ambalo limechipuka kwa jina ‘Marachi Boys’ ambalo kitovu chake ni mjini Busia.

Alisema vijana hao wamekuwa wakiwatisha watu katika eneo hilo.

Aidha Prof Kindiki amevitaka vyombo vya usalama katika eneo hilo kuchukua hatua za dharura dhidi ya kundi hilo na magenge mengine ya wahalifu.

Mbali na Busia, magenge hayo yanahangaisha wenyeji na wakazi wa kaunti za Bungoma na Vihiga.

“Wasiwasi umekuwepo kuhusu vijana wa ‘Marachi Boys’ huko Busia ambao wamekuwa wakiwatisha watu katika eneo hilo,” alisema Prof Kindiki akiwa katika eneobunge la Mumias Magharibi.

Pia alisema kuna genge jingine kwa jina ‘Jobless Group.

“Vijana kwenye magenge haya ya ujambazi eneo hili wabadilishe mienendo la sivyo wafahamu chuma chao ki motoni na watakumbana na mkono mrefu wa serikali,” akasema.

Aliyasema hayo Jumanne wakati wa uzinduzi wa ujenzi wa afisi ya Msaidizi wa Naibu Kamishna eneo la Musanda, Mumias Magharibi.

Mbunge wa eneo hilo, Johnson Naicca, alisifu ujenzi wa afisi hiyo, akisema ni kuleta huduma karibu na wakazi wengi ambao wamekuwa wakipata changamoto katika kupata huduma hizo.

“Wakazi wengi wamekuwa wakihangaika kupata huduma muhimu za serikali,” Bw Naicah akasema.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Punda wa Lamu wapumzika kiasi mwezi wa Ramadhani

Magwiji kuzalisha maharagwe ya jadi

T L