Kindiki atangaza Jumatano kuwa siku ya mapumziko, kuadhimisha Eid-ul-Fitri
NA CHARLES WASONGA
WAZIRI wa Usalama wa Ndani Kithure Kindii ametangaza Jumatano, Aprili 10, 2024 kuwa siku ya mapumziko.
Siku hiyo ni ya maadhimisho ya Siku Kuu ya Eid-ul-Fitr ambayo ni mwisho wa siku 30 wa mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan.
Waislamu kote nchini walianza mfungo huo mnamo Machi 10, 2024.
“Kwa mujibu wa mamlaka inayotokana na sehemu ya 2 (1) ya Sheria ya SikuKuu, natawaza Jumatano, Aprili 10, 2024 kama siku ya mapumziko kuadhimisha Siku Kuu ya Idd-ul-Fitri,” Prof Kindiki akasema kwenye taarifa fupi kwa vyombo vya habari.
Eid-ul-Fitri ni sikukuu muhimu ya kidini kwa Jamii ya Waislamu na kuadhimishwa katika mwisho wa mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan.
Mwezi huo ni wa tisa katika kalenda ya Kiislamu.
Sherehe hizo huanza kwa maombi maalum yanayojulikana kama; maombi ya Eid, yanayofanyika alfajiri baada ya mwezi kuonekana.