• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 5:17 PM
Kindiki awaonya wanasiasa dhidi ya malumbano ya kila mara Kisii

Kindiki awaonya wanasiasa dhidi ya malumbano ya kila mara Kisii

NA WYCLIFFE NYABERI

WAZIRI wa Usalama wa Ndani Kithure Kindiki amewaonya wanasiasa wanaochochea fujo katika Kaunti ya Kisii, akisema kuwa serikali itawaandama na kuwachukulia hatua za kisheria.

Prof Kindiki alisema wanasiasa hawafai kutumia vibaya uhuru wa demokrasia ya vyama vingi ili kusababisha machafuko ambayo yanahatarisha maisha ya Wakenya.

Akiongea mnamo Ijumaa alipozuru Kaunti ya Kisii, waziri huyo alisema serikali inafuatilia kwa karibu ongezeko la visa vya uhuni katika mikutano ya kisiasa eneo hilo.

Aliwahakikishia wakazi kuwa serikali inafanya juu chini kuzima mienendo hiyo mibovu.

“Siasa ni mapambano yanayofaa kufanywa kiustarabu. Kenya ni taifa la misingi ya demokrasia ya vyama vingi lakini hatutakubali watu wanaojificha nyuma ya siasa ili kuvunja sheria,” Prof Kindiki akasema.

Waziri huyo aliongeza kuwa utawala wa Rais William Ruto unachukulia swala la usalama wa taifa kuwa la umuhimu mno na kwa hivyo halifai kufanyiwa siasa kwa njia yoyote ile.

“Washikadau wote katika ulingo wa siasa na katika eneo hili wako huru kujihusisha na shughuli zao za kidemokrasia na hata kutofautiana kimawazo na kisera. Lakini hakuna anayeweza kujificha nyuma ya siasa kutekeleza uhalifu,” akaonya.

Aliwataka polisi pamoja na wakuu wao kutojihusisha kwa vyovyote katika siasa za nchi na badala yake akawataka wawatumikie Wakenya bila mapendeleo.

Ziara ya Prof Kindiki eneo la Kisii inajiri kufuatia matukio ya kutia aibu ambayo yamekuwa yakishuhudiwa kati ya wanasiasa wa mirengo kinzani katika siku za hivi punde.

Januari 2024, maisha ya raia wasiokuwa na hatia yaliwekwa hatarani baada ya risasi kufyatuliwa kiholela wakati Gavana wa Kisii Simba Arati na mbunge wa Mugirango Kusini Silvanus Osoro walitofautiana.

Na mnamo Februari 2024, Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu na kamishna mpya wa Kisii Joseph Kibet walitofautiana vikali na Bw Arati baada ya wawili hao kumlaumu gavana kuhusu fujo zilizokuwa zikiendelea Kisii.

Hata hivyo, gavana Arati alikana madai hao na kusema fujo za Kisii ziikuwa zikidhaminiwa na viongozi wanaoegemea serikali kuu, ambao alisema walikuwa wameweka zingatio kwa kusambaratisha utawala wake.

  • Tags

You can share this post!

Jamaa aamuru mke aache kazi alipoambiwa mdosi ni fisi sugu

Wakulima wa ndizi Taita Taveta watafutiwa soko kimataifa

T L