Habari za Kitaifa

Kindiki: Hakuna jinsi Upinzani unaweza kumshinda Ruto akiwa pande moja na Raila

Na KASSIM ADINASI October 14th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

NAIBU RAIS Profesa Kithure Kindiki amekariri kuwa upinzani hauna nafasi yoyote ya kushinda muungano wa Rais William Ruto na Kinara wa ODM Raila Odinga kwenye uchaguzi wa 2027.

Profesa Kindiki alisema upinzani kwa sasa umetambua hilo ndiposa viongozi wake sasa wamegeukia siasa za kikabila ili kukabili serikali.

Aliwarejelea viongozi wa upinzani kama waliojaa sarakasi na wale ambao wanabahatisha tu nafasi yao katika uchaguzi mkuu wa 2027.

“Viongozi wetu wawili wapo mbele na tunawafuata tukitambua kuwa hali ya baadaye ya nchi ni Serikali Jumuishi,” akasema Profesa Kindiki.

Alikuwa akiongea mjini Siaya wakati wa mchango wa kuyainua makundi ya wahudumu wa boda boda eneo katika hilo.

“Nawaona viongozi wa upinzani wakishiriki drama ya kujaribu kupimana na muungano wa Raila na Ruto. Wanaweza kutushinda kweli?” akauliza Profesa Kindiki.

Kauli yake inakuja baada ya aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua kusema kuwa upinzani utaungana na kuwashinda Raila na Rais Ruto.

Profesa Kindiki pia aliwashutumu viongozi wa upinzani kwa kutumia afya ya Bw Odinga kujipigia debe kisiasa.

Alisema kuwa ni aibu na ukosefu wa maadili kwa viongozi wa Afrika kuzungumzia afya ya kiongozi wa hadhi ambaye anaheshimika ndani na nje ya nchi kama Raila.

“Mzee Raila yuko salama na wale ambao wanamtakia maradhi na mauti si watu wazuri. Ni kinyume na tamaduni za Kiafrika kumtaka hata adui wako augue,” akasema Profesa Kindiki.

Alisema kuwa alikuwa amezungumza na Bw Odinga na waziri huyo mkuu wa zamani akamweleza kuwa yu salama kiafya.
“Nimeongea naye, hana neno, yu imara kiafya na anaendelea kupumzika,” akasema Prof Kindiki.

Chini ya Serikali Jumuishi, Naibu Rais alisema kuwa kila sehemu ya nchi itaendelezwa licha ya miegemeo yao ya kisiasa. Alisema kuwa kama viongozi, wanaunga mkono kwa dhati ushirikiano kati ya Rais na na Bw Odinga.

Profesa Kindiki alimsifu Gavana wa Siaya James Orengo kwa kukubali kuunga mkono Serikali Jumuishi na akaamua kuwa atahakikisha mwenyewe miradi ya kitaifa inakamilishwa katika kaunti hiyo.

“Orengo ni mwanasiasa, wakili mashuhuri na kiongozi ambaye alipigania ukombozi wa taifa hili. Tutashirikiana naye kuhakikisha kwamba Siaya inaendelea,” akasema naibu rais.

Kiongozi wa Wengi katika Seneti, Aaron Cheruiyot, naye alivamia upinzani akisema umemkosea heshima Raila.

“Kile ambacho aliyekuwa waziri mkuu amefanyia nchi, Gachagua hawezi kutimiza hata akiishi zaidi ya miaka 200,” akasema.

Kaunti ya Siaya ni kati ya zile ambazo zimenufaika na miradi mingi ya serikali ambayo ni ya thamani ya mabilioni ya hela.

Uga wa Siaya ni kati ya miradi ambayo imejengwa na serikali kwa kima cha Sh550 milioni.